‎Wataalamu wa Afya Waonya Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Antibayotiki Nchini .

0
92

‎Watafiti wa masuala ya afya nchini wameonya kuhusu ongezeko la visa vya matumizi mabaya ya dawa za kuua bakteria (antibayotiki) bila ushauri wa daktari, wakisema hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa usugu wa dawa na huenda ikaweka maisha ya binadamu na mifugo hatarini.

‎Onyo hilo lilitolewa wakati wa kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu nchini (KEMRI) jijini Mombasa, likiwakutanisha wataalamu wa afya, watafiti na wadau mbalimbali wa sekta ya afya.

‎Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa KEMRI, Dkt. Abdullahi Ali, alisema kuwa matumizi ya antibayotiki bila maelekezo ya wataalamu wa afya yameongezeka kwa kasi, hali inayotishia mafanikio yaliyopatikana katika matibabu ya magonjwa mbalimbali.

‎”Matumizi mabaya ya antibayotiki ni hatari kubwa kwa afya ya umma. Yanasababisha bakteria kuwa sugu, na kufikia hatua ambapo dawa zinazotumika sasa haziwezi tena kutibu maambukizi,” alisema Dkt. Ali.

‎Wataalamu hao walieleza kuwa miongoni mwa madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizo ni kuathirika kwa viungo vya ndani vya mwili kama figo na ini, pamoja na kuongeza gharama za matibabu kutokana na magonjwa kuwa magumu kutibika.

‎Dkt. Saumu Wayua, mtaalamu wa afya ya watoto katika Kaunti ya Mombasa, alionya kuwa watoto wako katika hatari zaidi kutokana na wazazi kuwapa antibayotiki bila vipimo au ushauri wa kitabibu.

‎“Watoto wanapopewa antibayotiki kiholela, kinga zao hushuka na baadaye wanapougua kweli, dawa hizo hazifanyi kazi ipasavyo,” alisema Dkt. Wayua.

‎Kwa upande wake, Profesa Sam Kariuki alibainisha kuwa magonjwa kadhaa ambayo awali yalikuwa rahisi kutibika yameanza kuonyesha usugu wa dawa, jambo linalotia hofu kwa mfumo wa afya nchini.

‎“Tunaona magonjwa kama nimonia, homa ya matumbo na maambukizi ya mfumo wa mkojo yakionyesha usugu mkubwa wa antibayotiki kutokana na matumizi mabaya ya dawa hizi,” alisema Profesa Kariuki.

‎Wataalamu hao sasa wanatoa wito kwa serikali kuongeza ufadhili kwa taasisi za utafiti kama KEMRI ili kuimarisha tafiti za kiafya, kubuni dawa mpya na kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti matumizi ya antibayotiki nchini.

LEAVE A REPLY