Leo, kama taifa, ni lazima tujiite kamkutano. Tujichune masikio, tujifurukute mioyo, na tujiulize: tunataka nini kama taifa? Ni kiongozi wa aina gani tunayemhitaji tunapoelekea uchaguzi wa mwaka 2027? Huu si wakati wa kelele za siasa au ahadi tamu zinazotoweka mara tu kura zinapohesabiwa. Ni wakati wa kujitazama kwenye kioo cha ukweli.
Tumeona mengi. Tumeshuhudia miradi mikubwa ikizinduliwa kwa mbwembwe, wakuu wakihutubia kwa maneno ya matumaini, mikono ikipigwa makofi na matumaini yakiibuka mioyoni mwa wananchi. Lakini baada ya muda mfupi, yale matumaini yanayeyuka — miradi inasalia kuwa magofu, misingi iliyowekwa inafunikwa na vumbi, na picha za uzinduzi ndizo zinabaki kwenye mabango.
Swali linajitokeza: zile fedha zinazotengewa miradi hiyo huwa zinaenda wapi? Ni kwa nini miradi moja huzinduliwa mara mbili, mara nyingine hata mara tatu? Kwa nini hakuna anayewajibika, ilhali kiongozi huyo huyo hurudi tena miaka michache baadaye, akiwa na maneno yale yale, akituomba kura kwa matumaini mapya?
Wakati umefika wa wananchi kuamka. Uongozi si uimbaji wa ahadi; ni utekelezaji wa wajibu. Lazima tuwe na ujasiri wa kuwauliza viongozi wetu maswali magumu. Kama mradi haujakamilika, kwa nini? Kama fedha zimetolewa, ziko wapi? Na kama hakuna majibu, basi tusitoe kura zetu kama zawadi kwa kutojali.
Kamkutano wa taifa unaanza leo — si ukumbi wa hotuba, bali ni maamuzi ya kila mwananchi moyoni mwake. Maamuzi ya kusema: hatutadanganywa tena, hatutasahau tena, hatutazinduliwa tena kwa maneno matupu.
Uongozi bora haujengwi kwa maneno, unajengwa kwa matendo. Na mwaka 2027, kura zetu ndizo zitakazosema — tumeelewa, tumejifunza, na sasa tunachagua kwa akili, si kwa kelele.



