TAHARIRI: WAKATI WA VIONGOZI KUACHA MANENO, WAFANYE VITENDO
Ni wakati sasa wa viongozi wetu kuacha siasa za maneno matupu na kujikita kwenye utendakazi. Kila baada ya muda mfupi tunashuhudia wimbi la viongozi kupiga kampeni, si kwa ajili ya uchaguzi ujao, bali kwa kutangaza mipango yao isiyotekelezeka.
Wamegeuza majukwaa ya umma kuwa sehemu za kujisifu badala ya kutoa matokeo halisi ya kazi. Wanasema watafanya, watajenga, wataboresha lakini wananchi bado wanasubiri kuona matunda ya ahadi hizo ambazo zimegeuka kama wingu lisilonyesha mvua.
Kiongozi wa kweli hatangazi kazi, bali vitendo vyake huzungumza vyenyewe. Mwananchi hafai kushawishiwa na hotuba ndefu wala mabango yenye maneno makubwa, bali na matokeo yanayoonekana barabara zilizokamilika, shule zenye vifaa, hospitali zinazotoa huduma bora, na vijana walioajiriwa. Hayo ndiyo maendeleo tunayohitaji kuona, sio miradi ya karatasi inayozinduliwa kila msimu wa siasa.
Ni aibu kwa kiongozi kujiita kwa mikutano, kujisifu hadharani, na kujipa sifa ambazo hazina mashiko. Mkenya wa leo si yule wa jana anatambua ukweli, anaona, na anauliza maswali.
Tunataka kuona utekelezaji wa manifesto, sio maelezo mapya kuhusu mipango mipya ambayo itasahaulika kesho. Kila kiongozi aliyechaguliwa ana jukumu la kuonyesha matokeo ya ahadi alizotoa, sio kutumia kila jukwaa kuanza kampeni za mapema.
Wakati umefika wa vitendo kuzungumza badala ya maneno. Maendeleo hayahitaji matangazo yanahitaji utendaji, nidhamu, na uwajibikaji. Kiongozi anayefanya kazi kwa moyo, wananchi wenyewe watampongeza bila yeye kujipigia debe. Wataona mabadiliko katika maisha yao na kusema, “Ndiyo huyu kiongozi wetu wa mfano.”
Kwa hivyo, viongozi waache kampeni zisizoisha. Waache kujitafutia umaarufu kwa maneno, badala yake wajitafutie heshima kwa kazi. Wananchi wanataka kuona maendeleo yanayogusa maisha yao moja kwa moja, sio hotuba zenye ahadi hewa. Wakati wa maneno umekwisha



