Katika siku za karibuni, taifa limejionea mwenendo unaotia wasiwasi katika maandalizi ya uchaguzi ndogo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kasipul, Malava, Magarini, Ugunja, Baringo, Narok, Kisii na sehemu nyingine kadhaa. Badala ya kuwa chaguzi za kawaida za kujaza nafasi zilizoachwa wazi, zimegeuka kuwa uwanja wa kuonyeshana ubabe wa kisiasa na maonyesho ya nguvu kutoka kwa wanasiasa wakubwa.
Tumeona ndege za serikali na misafara mikubwa ya magari ikizunguka nchi nzima, zikisafirisha viongozi kufanya kampeni katika kila kona. Swali la msingi ni hili ikiwa gharama hizi ni kubwa kiasi hiki kwa uchaguzi mdogo, itakuwaje ikifika uchaguzi mkuu wa 2027?
Wakati mabilioni yanatumika kufanya misafara ya kisiasa angani na barabarani, miradi mingi muhimu imekwama baadhi zikihitaji fedha kidogo tu kukamilika. Ni halali kujiuliza ni kwa nini nguvu na fedha hizi zisitumike kwenye maendeleo ya wananchi badala ya kampeni za viti vidogo vya ubunge? Kama kweli serikali inajiamini na inaaminiwa na wananchi, kwa nini isiache wananchi wachague yule wanayemtaka bila shinikizo la kampeni nzito?
Pia tumeona matukio ya pesa kutolewa hadharani na baadhi ya viongozi wakati wa kampeni, jambo linaloibua swali lisiloweza kuepukika pesa hizi zinatoka wapi, na kwa malengo gani hasa? Matumizi ya fedha katika kampeni yanazidi kuacha doa katika safari yetu ya kidemokrasia.
Aidha, visa vya uchafuzi wa kisiasa vimeongezeka kutumika kwa makundi ya kuvuruga mikutano ya wapinzani, na hata matukio ya risasi kurushwa hadharani. Haya yote yanaonyesha jinsi siasa zetu zinavyozidi kupoteza maadili na misingi ya heshima na ushindani wa hoja.
Demokrasia ya kweli inahitaji ushindani wa sera, sio maonyesho ya nguvu. Inahitaji kuwapa wananchi nafasi ya kuchagua bila hofu, bila kununuliwa, bila kushinikizwa na misafara inayotumia fedha ambazo zingesaidia huduma za umma.
Kadri tunavyoelekea 2027, ni lazima tujiulize Je, tunaelekea kwenye uchaguzi wa demokrasia, au maonesho ya ubabe? Na je, viongozi wako tayari kuweka maslahi ya taifa mbele ya maslahi yao binafsi?



