Tukio la jana kule Kariobangi limeacha doa jeusi katika safari ya taifa letu kuelekea ustaarabu. Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi—vitoza machozi vilivyopenya mpaka ndani ya kanisa, mahali patakatifu ambapo watu hawakuja kwa siasa, hawakuja kwa vurugu, bali kwa ibada. Watoto, akinamama, na waumini waliokuwa kwa ajili ya amani walijikuta wakikimbizwa kama wahalifu. Tunauliza: Tunaishi katika taifa lipi?
Kanisa sio uwanja wa siasa. Watoto wasiostahili hata kusikia kishindo cha siasa wamejikuta wakivuta gesi inayochoma macho na koo—gesi iliyorushwa na walinzi wa usalama wanaopaswa kulinda raia bila ubaguzi. Idara ya polisi lazima ijirekebishe. Hakuna taifa linaloendelea kwa vitendo vya kutumia nguvu kiholela bila taarifa, bila taratibu, bila hata hisia za ubinadamu.
Waliorusha mabomu hayo wanapaswa kueleza: Ni amri gani waliyopewa? Ni akili gani iliwaruhusu kulenga eneo la ibada? Hata kama kulikuwa na wahuni nje, hata kama kulikuwa na msuguano wa kisiasa, sheria ni moja: siasa zikome kanisani.
Kisha kuna swali zito zaidi: Je, huku ndiko tunakoelekea tunaposema tunataka kufikia “Singapore”? Taifa lisiloweza kudhibiti wahuni kabla hawajazidi polisi, taifa linalojua vizuri kuwa goons ni biashara ya baadhi ya wanasiasa lakini linanyamaza kimya—taifa hili linaelekea wapi?
Tahariri hii inasema wazi: Wahuni hawa waitwao goons ni mradi wa mtu. Hawaibuki tu kutoka hewani. Wana wafadhili, wana waendeshaji, na wana masilahi ya kisiasa. Na vyombo vya usalama wanawajua—kwa majina, kwa makazi, na kwa mabwana wanaowatuma. Hili si taifa tunalotaka, na hili si taifa linaloweza kusimamia uchaguzi huru wakati kampeni rasmi bado hazijaanza lakini vikundi vya fujo tayari vinajengwa bila kudhibitiwa.
Ni wakati wa serikali na vyombo vya usalama kusimama kidete: Wadhibiti wahuni, waheshimu nyumba za ibada, wawalinde wananchi bila upendeleo. Maana kama leo kanisa halina usalama, basi kesho hata shule, hospitali, na masoko yatakuwa uwanja wa mabomu.
Taifa haliwezi kujengwa juu ya fujo, vitisho na sarakasi za wahuni wanaolishwa na siasa chafu.
Leo tumesema: Siasa zikome kanisani. Polisi wajiangalie. Na wanasiasa waache kutumia goons.




Tunalaani na kukemea vikali