SHA Inatufaa au Inatufyonza?

0
150

Mwaka bado haujakamilika tangu kuzinduliwa kwa Mfumo mpya wa bima ya afya –Social Health Authority (SHA) mnamo tarehe 1 Oktoba, lakini tayari tumeshuhudia sakata ya mabilioni ya pesa ikiyoyoma kutoka kwa hazina ya umma hadi mifuko ya wamiliki wa hospitali kwa njia za utapeli.

Wakenya walilitarajia jambo kama hili kutokea – si kwa sababu ni halali, bali kwa sababu historia yetu imetufundisha kutoamini mifumo mipya, hasa ikizinduliwa bila maandalizi ya kutosha na uangalizi madhubuti. Lakini walichokosa kujua ni ni lini ufisadi huo ungeanza Jibu sasa liko wazi umeanza hata kabla mfumo huu haujatimiza mwaka mmoja.

Rais William Ruto alipotangaza kuzinduliwa kwa SHA, alisisitiza kuwa mfumo huo unakuja kuziba mianya yote ya ulaghai iliyokuwepo katika NHIF. Aliahidi mageuzi ya kweli, uwazi na ufanisi. Lakini leo tunapojitazama kama taifa, tuna maswali mazito yanayohitaji majibu ya dharura

Kama SHA ndiyo mfumo bora tuliouahidiwa, kwa nini hospitali zinadaiwa na serikali kwa huduma ambazo hazikutolewa?
Mbona wagonjwa hewa, upasuaji hewa, na malazi hewa vinaendelea kuripotiwa?
Kwa nini mfumo uliogharimu umma shilingi bilioni 104 sasa unapoteza zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa ulaghai?

Waziri wa Afya, Aden Duale, amekiri wazi kuwa baadhi ya hospitali zimerekodi huduma feki: wengine wanaripoti kuwa mgonjwa alilazwa huku akiwa nyumbani, wengine wamesema walifanya upasuaji wa mara tano kwa mama aliyejifungua jambo lisilo na mantiki yoyote. Hii ni kashfa ambayo haijawai kuonekana.

Ni wapi tatizo linaanzia?, tatizo linaanzia mbali. Zabuni ya kuunda mfumo wa SHA – iliyogharimu bilioni 104 – ilikabidhiwa kwa kampuni moja bila ushindani wa wazi. Sheria hazikuzingatiwa. Huu ndio ulikuwa uhalisia wa “mwanzo mpya” uliopigiwa debe. Ufisadi uliupenya mfumo huu kabla hata wagonjwa hawajaanza kunufaika nao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA, Bi. Mercy Mwangangi, kupitia tangazo rasmi la serikali, ametaja vituo 45 ambavyo havitaruhusiwa kupokea malipo ya SHA kwa sasa. Tunashukuru kwa hatua hiyo, lakini tunahoji: Je, ni hivyo vituo pekee? Au kuna vingine “vimekingwa” kwa sababu ya ushawishi wa kisiasa na ukaribu na mamlaka?

Ni lini uchunguzi wa kweli utafanywa?
Ni akina nani waliohusika katika kuiba fedha hizi, na watawajibishwa lini?
Ni kwa nini SHA haiwezi kulinda pesa za mlipa ushuru dhidi ya matapeli wa sekta ya afya?
Na je, ni kwa nini serikali haikuimarisha NHIF badala ya kujenga mfumo mpya kutoka mwanzo kwa gharama ya mabilioni?

Wakenya tayari wanalipa ushuru mkubwa sasa wakipewa mzigo mwingine wa kutegemea mfumo wa SHA ambao hauwezi hata kulinda pesa zao.
Nitasema hivi serikali isicheze shere katika mambo muhimu kama ya afya wakenya wanatka kuona wote wanahusika kufunguliwa mashtaka.

LEAVE A REPLY