Kikosi hicho kitahusisha taasisi mbalimbali za serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa.
Kikosi hicho sasa kitakuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kuimarisha juhudi za taifa za kukomesha ufisadi, utakatishaji wa fedha na uhalifu wa kiuchumi.
Kikosi hicho (Multi-Agency Team – MAT), kinakuja siku chache tu baada ya Rais kutoa onyo kali kwa maafisa wa serikali wanaojihusisha na vitendo vya kifisadi.
Rais Ruto alieleza kuwa lengo kuu la kikosi hicho ni kuimarisha ushirikiano, uratibu na mshikamano kati ya taasisi kuu za serikali zinazopambana na ufisadi, utakatishaji wa fedha haramu na uhalifu unaohusiana na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Taasisi zitakazoshiriki katika MAT ni pamoja na:
Afisi ya Rais
Afisi ya Mwanasheria Mkuu
Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS)
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC)
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI)
Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP)
Kituo cha Kuripoti Masuala ya Fedha (FRC)
Mamlaka ya Kukamata Mali (ARA)
Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA)
Benki Kuu ya Kenya (CBK)
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA)
Aidha, taasisi nyingine zinaweza kuongezwa katika kikosi kazi hicho pale inapohitajika, kwa mujibu wa mamlaka ya Rais.
Majukumu Muhimu ya [MAT] ni ikiwemo;
Kukuza ushirikiano wa kisekta kati ya taasisi za serikali na wadau wengine muhimu katika vita dhidi ya ufisadi.
Kuratibu na kuendesha oparesheni za pamoja za kushughulikia kesi za ufisadi, uhalifu wa kifedha na unyakuzi wa mali ya umma.
Kusaidia utekelezaji wa sheria mpya, ikiwemo Sheria ya Migongano ya Maslahi ya mwaka 2025 na marekebisho ya Sheria ya Mapato Yanayotokana na Uhalifu (Pocamla).
Kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kufuatilia na kurejesha mali zilizopatikana kwa njia ya kifisadi kutoka mataifa ya kigeni.
Kuelimisha umma kuhusu madhara ya ufisadi na kuhimiza ushiriki wao katika kuzuia uovu huo.
Kubadilishana mbinu bora za kiufundi na kiuchunguzi kati ya taasisi mbalimbali.
Kuwezesha upatikanaji wa rasilimali muhimu za kifedha, kiufundi na kiteknolojia kwa taasisi shiriki.
Rais Ruto alieleza kuwa fedha za kuendesha shughuli za MAT zitapatikana kutoka bajeti za kawaida za taasisi shiriki, huku serikali ikiwa tayari kutoa msaada wa ziada pale utakapohitajika.



