Matamshi ya Rais hivi majuzi kwamba baadhi ya wabunge wamepokea hongo ya kiwango kikubwa cha pesa ili kufanya maamuzi katika Bunge la Kitaifa si jambo la kawaida ni tetesi nzito. Swala hili limezua gumzo kali miongoni mwa wananchi, wadau wa haki na demokrasia, huku baadhi ya wabunge wakionekana wakifoka kwa hamaki na kujinasibu kuwa wana mamlaka hata juu ya asasi kuu ya serikali yaani Executive.
Tujiulize hivi; Kama kweli kuna wabunge waliohongwa ili kupitisha au kupinga hoja fulani bungeni, je, hili si kosa la jinai? Je, huu si usaliti kwa wananchi waliowachagua? Ni kwa nini Rais, ambaye anao vyombo vyote vya dola mikononi mwake, anachagua kulisema hili kwa njia ya kisiasa kwenye majukwaa badala ya kulishughulikia kisheria? je Rais ameliserma tamko hili kutoka moyoni na matumaini dhidi ya mwananchi na katika vita kuhusu ufisadi ama ni kelele tu za kisiasa zinazopita?
Rais ajue kwamba wakenya hawataki tena kusikia hotuba zenye maneno mazito lakini zisizo na matokeo. Wananchi wanataka kuona vitendo. Wanataka kuona mafisadi wakikamatwa, wakifikishwa mahakamani, na wakifungwa iwapo watapatikana na hatia. Wanataka kuona mali ya umma iliyoibwa ikirejeshwa kwa manufaa ya wananchi, si kusikika tu kwenye mikutano ya kisiasa.
Ni aibu kwamba wawakilishi wa wananchi, ambao wanapaswa kuwa nguzo ya maadili na uadilifu, sasa wanatuhumiwa kuwa wauzaji wa dhamira zao kwa hela chafu. Mbona wabunge wanakimbilia kujitetea kwa sauti kali badala ya kutaka uchunguzi wa wazi na wa haki? Wanaogopa nini? Je, waliguswa na matamshi ya Rais kwa sababu yana ukweli fulani ndani yake?
Kwa upande mwingine, ni lazima pia tujiulize: Kama Rais amefikia kiwango cha kutoa tuhuma nzito kama hizi hadharani, je, ana ushahidi? Na kama anao, ni lini utawekwa wazi na kuwasilishwa kwa taasisi husika ili hatua zichukuliwe?
Ufisadi ni donda ndugu katika taifa letu, na haufai kupambwa wala kuchezewa kisiasa. Rais, akiwa kiongozi wa nchi na mlezi wa katiba, hana budi kuchukua hatua thabiti, zisizo na upendeleo. Vinginevyo, wananchi wataendelea kuona haya matamshi kama sarakasi za kisiasa zenye lengo la kuwaburudisha tu kwa muda mfupi.
Rais ana mamlaka ana nguvu na kila anachokihitaji kukabiliana na ufisadi wakenya wanasubiri kuona vitendo.



