Mombasa /KENYA
Polisi katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, wamefanikiwa kuwakamata washukiwa wa wizi kufuatia operesheni ya usiku iliyoendeshwa baada ya kupokea simu ya dharura kutoka kwa mkazi wa eneo la Shonda.
Akizungumza na wanahabari, Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Likoni, Joseph Mutungi, alisema kuwa walipokea simu ya dharura majira ya saa tatu usiku ikieleza kuwa watu wasiojulikana walikuwa wamevamia duka la mfanyabiashara kwa nia ya kuiba mali.
Alisema kuwa maafisa wa polisi waliitikia wito huo kwa haraka na kufika katika eneo la tukio, ambapo walikumbana na kundi la watu wanane waliokimbia walipowaona askari. Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya washukiwa hao, na katika mchakato huo baadhi yao walijeruhiwa kwa risasi.
“Maafisa wetu walifanikiwa kumkamata mshukiwa mmoja papo hapo, huku wengine waliokuwa wamejeruhiwa kwa risasi wakikamatwa baadaye,” alisema Kamanda Mutungi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, hadi kufikia sasa washukiwa wanne wamekamatwa, na walinaswa wakiwa na simu za rununu zinazoaminika kuwa mali ya wizi. Mshukiwa mmoja pia aliwaongoza polisi hadi kwa mshukiwa mwingine, ambapo mali zaidi zilipatikana.
Katika operesheni hiyo, polisi walinasa:
Simu kadhaa za rununu
Mapanga (machetes)
Crowbars mbili
Suruali ya kijeshi
Mitungi ya gesi
Gunia la mchele
Pikipiki tatu (motorbikes) ambazo zinadaiwa kuwa ndizo zinazotumiwa na washukiwa kutekeleza uhalifu.
Kamanda Mutungi alibainisha kuwa operesheni za kuwasaka washukiwa wengine waliotoroka bado zinaendelea, na akawahakikishia wakazi wa Likoni kuwa usalama wao umepewa kipaumbele.
Aidha, alitoa onyo kali kwa magenge ya kihalifu yanayoendesha shughuli haramu katika eneo la Likoni, akisisitiza kuwa polisi hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayehusishwa na uhalifu.



