Parachichi Kisii: Dhahabu Mpya Inayochipua Polepole

0
155
PICHA /Avokado

Katika maeneo ya Kisii, parachichi sasa limepata umaarufu mpya kama bidhaa ya thamani, inayochipua polepole kama dhahabu mpya. Miaka michache iliyopita, parachichi halikuwahi kuwa bidhaa ya kawaida ya kununua sokoni, bali lilikuwa ishara ya ukarimu na heshima katika jamii ya Abagusii.

Katika utamaduni wa zamani wa Omogusii, kupokea mgeni kulihusisha zawadi ya parachichi na ndizi, ikiwakilisha baraka na ukarimu wa familia. Mgeni alikaribishwa kwa kipande kilichokatwa kwa ustadi cha parachichi tamu, pamoja na chai au uji mzito uliomiminiwa kikombeni. Baada ya chakula, mgeni aliaga akiwa na mzigo wa parachichi na ndizi kama zawadi ya nyumbani, ishara ya mshikamano wa kijamii.

Lakini sasa hali imebadilika hali ngumu ya  kiuchumi imefanya parachichi kuwa bidhaa ya gharama kubwa. Hivi sasa, bei ya parachichi kubwa la familia katika maeneo ya Kisii inaweza kufikia kati ya Ksh 70 hadi Ksh 100, hali ambayo ilidhihirika kuwa nadra miaka iliyopita. Zaidi ya hayo, mapera na matunda mengine ya asili—yanauzwa kiholela mitaani kama bidhaa za biashara, jambo ambalo halikuwahi kutokea zamani.

Mabadiliko haya yamechangiwa na hali ya umaskini inayokumba sehemu kubwa ya jamii, na yanaashiria mwelekeo wa kupungua kwa utamaduni wa ukarimu na mshikamano wa jamii ya Abagusii. Ikiwa hali hii itaendelea, kuna hatari ya parachichi kuonekana kama bidhaa adimu, na wengi kupoteza uwezo wa kuipata.

Hali hii inatoa changamoto kubwa kwa jamii kuhusu uhifadhi wa tamaduni zao na jinsi zinavyoathiri maisha ya kila siku. Je, parachichi bado ni sehemu ya maisha yenu? Bei ikoje katika maeneo mengine? Ni muhimu kushirikiana na kuangalia njia za kuhifadhi na kukuza utamaduni wetu pamoja na kuboresha hali ya maisha ya watu.

LEAVE A REPLY