Ufisadi umekuwa saratani sugu inayokula Afrika kutoka ndani.Kila mwaka, bara hili linapoteza mabilioni ya fedha kupitia mikono ya wachache walioaminiwa kuwa walinzi wa maliasili za wananchi. Wakati wananchi wanalia njaa, kukosa dawa hospitalini, na kukwama kwenye miundombinu duni, viongozi wao wanatajirika katika muda usioelezeka. Ni taswira ya kusikitisha, lakini pia ya kuudhi.
Afrika ni bara lenye hazina kubwa ya rasilimali madini, mafuta, ardhi, nguvu kazi lakini limegeuka ombaomba wa kimataifa. Serikali nyingi hukopa kutoka Benki ya Dunia (World Bank) na IMF, kwa matumaini ya kuendeleza miradi ya wananchi. Lakini swali kuu linabaki: Je, fedha hizi zinafika kwa mwananchi? na Jibu, kwa masikitiko, ni hapana.
Asilimia kubwa ya mikopo hii imekuwa ikitoweka kupitia mifuko ya wezi sugu wa serikali, wanaojificha nyuma ya suti nadhifu, maneno matamu, na mikataba ya kifisadi. Wananchi wanabaki na madeni, lakini hawapati faida.
Kenya ni kielelezo hai cha janga hili. Eurobond—zile pesa ambazo hadi leo hakuna anayejua safari yake kamili. Fedha za COVID-19 – zilitoweka kama mvuke wa maji. Sakata baada ya sakata, uchunguzi unaanzishwa, kamati zinaundwa, ripoti zinaandikwa… lakini mwisho wote ni ule ule: ukimya. Washukiwa wanacheka vijijini wakila pesa za wanyonge. Wananchi wanabeba mzigo wa kodi, lakini hawana pa kukimbilia.
Tofauti na Afrika, mataifa mengine hayacheki na ufisadi.
Kule uchina ukipatikana na chembe ya ufisadi, hukumu ni kifo kwa risasi hadharani. Mantiki ya taifa hilo ni rahisi: ukimwibia mwananchi mmoja, umewaibia mamilioni; basi adhabu iwe fundisho kwa wote
Baadhi ya mataifa ya Kiarabu hutumia adhabu kali kama kunyongwa au kifungo cha maisha bila fursa ya huruma. Huko,CORRUPTION IS NOT A JOKE.
Katika bara letu, ukijaribu kupeleka mswada wa adhabu kali dhidi ya mafisadi bungeni, hata milango ya Bunge haitafunguka. Utazuiwa kabla hujafika lango la kuingia Kiongozi gani ataunga mkono sheria inayoweza kumwumbua? Hakuna. Wengi wao ni wanaonufaika na mfumo waliouunda wenyewe.
Ni nani aliyeilaani Afrika? Ni nani aliyeweka giza katika roho za viongozi wake?
Nitasema kwamba ikiwa tunataka kukabiliana ufisadi sharti sheria kali za zipitishwe.



