Ni Nini Wabunge Wengine Wanashindwa Kukifanya ?

0
114
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro

Kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakiuliza Kazi ya mbunge ni ipi hasa? Je, ni kuhudhuria vikao vya Bunge pekee, au ni kuhakikisha maisha ya wananchi yanabadilika moja kwa moja? Tukitazama mfano wa Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, maswali mengi zaidi yanajitokeza hasa tukiwalinganisha na wabunge wengine kote nchini.

Kwa nini katika maeneo mengi bado tunaona shule zisizo na madarasa ya kutosha, ilhali Kiharu wanafunzi wa shule za kutwa wanalipa shilingi 500 tu kwa muhula na bado wanapata chakula shuleni? Je, wabunge wengine wanashindwa kuelewa kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo, au wanachagua tu kutoipa kipaumbele?

Kwa nini bado kuna maeneo ambako wazazi wanalia kila muhula kwa ada ya shule, ilhali Kiharu walimu na wanafunzi wanapewa motisha, tuzo na hata safari za kielimu kama Dubai na Malaysia? Je, wabunge wengine wanashindwa kuthamini walimu na wanafunzi wao, au wanashindwa kupanga matumizi bora ya fedha za NG-CDF?

Kwa nini katika baadhi ya maeneo barabara bado hazipitiki, hasa wakati wa mvua, ilhali Kiharu miundombinu inaendelea kuboreshwa kila mwaka? Je, wabunge wengine wanashindwa kufuatilia miradi hadi ikamilike, au wanaridhika na kuweka mawe ya msingi kwa ajili ya kamera pekee?

Kwa nini wananchi wengi bado wanalalamika kuwa hawaoni wabunge wao isipokuwa wakati wa kampeni, ilhali Ndindi Nyoro ameonekana mara kwa mara akihusishwa moja kwa moja na miradi ya wananchi? Je, tatizo ni kukosa muda, au kukosa dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi?

Je, ni kwa sababu wabunge wengine hawapewi pesa za kutosha? Ukweli ni kwamba wabunge wote hupokea mgao unaofanana wa NG-CDF. Kama hivyo ndivyo, basi swali kubwa linabaki: kwa nini matokeo ni tofauti sana? Je, tatizo ni matumizi mabaya ya rasilimali, au ni kukosa maono?

Kwa nini siasa kwa wabunge wengi imekuwa ni kelele, lawama na migawanyiko, ilhali Kiharu wameona mfano wa mbunge aliyotenga siasa na maendeleo? Je, wabunge wengine wanashindwa kuelewa kwamba maendeleo hayana chama wala rangi ya kisiasa?

Tahariri haimpigii kampeni mbunge huyu bali inaweka sifa panapostahili chanda chema huvikwa pete.

LEAVE A REPLY