Katika taifa linalodai kuwa la kidemokrasia, lenye katiba ya mwaka 2010 iliyojaa maneno matamu kuhusu utu wa binadamu, usawa wa raia na mshikamano wa kitaifa ni aibu kubwa, fedheha kuu, na doa lisilofutika pale ambapo viongozi waliochaguliwa kwa kura ya umma wanageuza majukwaa kuwa maabara za kuchochea chuki za kikabila.
Kauli ya Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga, inayodai kuwa kifo cha Rt. Hon. Raila Amolo Odinga kilikuwa “jibu la Mungu kwa maombi ya Wakiukuyu” ni mashambulizi ya kimaadili, dhihaka kwa wafiwa, na kisigino cha kisiasa kisichostahili kusimamia hata kivuli cha uongozi.
Acha niseme kwamba Mauti si nafasi ya kupiga siasa. Mauti si muda wa kupigia siasa za eneo. Mauti ni kioo kinachotuonyesha udogo wetu mbele ya Muumba, na ni kipindi cha kutafakari urithi wa walioondoka.
Kwa mtu wa cheo cha gavana kusema kwa mzaha kwamba Mungu “alichukua” Raila kwa sababu ya malalamiko ya watu wa Mlima Kenya ni uthibitisho wa uozo wa kisiasa ulioota mizizi ndani ya baadhi ya viongozi wetu.
Hii si siasa. Huu ni udhaifu wa utu. Hii ni siasa ya maiti, na walio hai lazima waikemee kwa nguvu zote.
Gavana Kahiga si mgeni katika siasa. Anajua uzito wa maneno. Kwa hivyo, kauli yake haipaswi kuchukuliwa kama matamshi ya hasira, au kejeli ya msimu. Haya ni matamshi ya makusudi, yaliyopangwa kuchochea hisia za kieneo, kwa lengo la kuendeleza simulizi hatari kuwa jamii fulani ndio “adui” wa jamii nyingine. Huu ni ugaidi wa kisaikolojia kwa raia wanaotafuta mshikamano wa kitaifa.
Je, huyu si yule Mutahi Kahiga aliyeingia mamlakani baada ya kifo cha Dkt. Wahome Gakuru? Je, hakukalia kiti cha ugavana kwa sababu ya msiba? Aliposimama kuapishwa, taifa lilikaa kimya, likamheshimu. Leo hii, anatamka maneno ya dharau kwa marehemu Raila mtu ambaye kwa zaidi ya miongo minne, alijitoa kupigania uhuru wa pili wa taifa hili?
Raila Amolo Odinga si jina la kawaida katika historia ya Kenya. Ni sura ya mateso ya magereza ya Moi. Ni damu ya Saba Saba. Ni sauti ya walioibiwa kura. Ni jicho la waliojeruhiwa na polisi kwa maandamano ya haki. Kupenda au kutopenda, Raila alikuwa sehemu ya dhamira ya taifa hili – kiashiria kwamba kuna watu walio tayari kuvunjika kwa ajili ya haki.
Kumkejeli mtu kama huyu baada ya kifo ni kudharau historia. Ni kutukana taifa. Ni kusaliti maadili ya Kiafrika, ambapo hata katika vita vikuu vya kikabila, waliokufa waliheshimiwa.
Kauli za Kahiga si za kupuuzwa. Zinaweza kuonekana kama mzaha, lakini ni mbegu za chuki, na ikiwa hazitazimwa mapema, zitachoma taifa zima. Tunapochukulia kwa urahisi kauli kama hizi, tunakaribisha hasira za mitaani, ghasia za uchaguzi, na migawanyiko ambayo huacha majeraha ya vizazi.
Hatupaswi kumwambia aombe msamaha tu lazima awajibishwe. Ashtakiwe kwa kuchochea chuki za kikabila. Ashtakiwe kwa kutumia mamlaka vibaya kueneza siasa za mauti.
Gavana Kahiga na viongozi wengine wa fikra potovu waelewe hivi kifo hakina kabila. Hakibagui Mlima wala Ziwa. Kifo ni kiapo cha mwanadamu yeyote. Kifo cha Raila ni kivuli cha vifo vyetu sote. Leo hii ni yeye, kesho ni sisi. Na ardhi hiyo hiyo inayotumia



