MAHAKAMA KUU YASITISHA UTEKELEZWAJI WA SHERIA YA MATUMIZI YA MTANDAO.

0
83

Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi alisimamisha utekelezaji wa baadhi ya vifungu muhimu vya Sheria vilivyowekwa saini na Rais William Ruto katika ikulu ya Nairobi tarehe 15/10/2025.

Baadhi ya sheria hizo ni uhalifu wa matumizi ya mitandao ambapo jaji huyo wa mahakama kuu aliweka kikomo kwa muda utekelezaji wa sheria hizo hadi pale kesi iliyowasilishwa ya kupinga uhalali wake kikatiba itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Mnamo Jumatano, Oktoba 22.Mugambi alitoa amri ya muda kusitishwa utekelezaji wa vifungu vya kisheria hasa kifungu cha 27(1)(b), 27 (1)(c) na 27(2) vya sheria hiyo kabla ya kesi iliyowasilishwa mahakamani itakapoamuliwa.

Vifungu hivyo vilikuwa vimezua wasiwasi miongoni mwa makundi ya haki za binadamu nchini Kenya kuhusu athari zake kwa uhuru wa kujieleza na haki za kidijitali.

Amri hizo zilitolewa kufuatia ombi la dharura lililowasilishwa na mwanamuziki wa injili na mwanaharakati Reuben Kigame, kwa ushirikiano na Tume ya kutetea haki za binadamu nchini (KHRC).

Katika uamuzi wake, Mugambi alisema “Kabla ya kusikilizwa na kuamuliwa kwa ombi hili, amri ya muda inatolewa kusitisha utekelezaji, uanzishaji na uendeshaji wa vifungu vya 27(1)(b), (c), na (2) vya Sheria ya Uhalifu wa Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni (Marekebisho) ya mwaka 2025.”

Vifungu vilivyositishwa vinahusiana na uhalifu wa unyanyasaji mtandaoni, ambavyo vinapiga marufuku kwa mawasiliano ya kielektroniki yanayoweza “kumdhuru mtu mwingine” au yaliyomo “yasiyo na maadili au yanayokera kupita kiasi.”

Kulingana na Kifungu cha 27 cha sheria hiyo, mtu atakayepatikana na hatia anaweza kutozwa faini ya shilingi milioni 20, au kufungwa hadi miaka 10, au vyote viwili.

Sheria hiyo imezua hisia mseto miongoni mwa Wakenya na wasanii mbalimbali huku baadhi wakisema ni hatua nzuri ya kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ilihali wengine wakidai kuwa inapaswa kupitiwa upya kwani baadhi ya vifungu vinaweza kutumika kukandamiza uhuru wa kujieleza.

LEAVE A REPLY