Madini Ya Dhahabu Ya Kakamega Yawe Baraka Isiwe Laana

0
100

Habari za kupatikana kwa madini ya thamani, hasa dhahabu, katika Kaunti ya Kakamega zimeibua matumaini makubwa miongoni mwa wananchi na serikali. Wengi wanaona huu kuwa mwanzo wa neema, ajira, maendeleo na mapato makubwa kwa taifa. Hata hivyo, historia ya bara la Afrika inatukumbusha kuwa utajiri wa madini mara nyingi umekuwa chanzo cha machozi, umaskini, na vita. Ni lazima tujiulize: je, dhahabu ya Kakamega itakuwa baraka kwa Wakenya, au itageuka kuwa laana kama ilivyotokea katika mataifa mengine?

Katika nchi nyingi za Afrika, upatikanaji wa madini umeibua migogoro mikubwa. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa mfano, ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini kama cobalt, almasi na dhahabu. Lakini badala ya neema, utajiri huo umekuwa chanzo cha vita vya wenyewe kwa wenyewe, uporaji wa mali, na uingiliaji wa mataifa ya kigeni yanayofadhili makundi ya waasi kwa tamaa ya kupata madini kwa bei rahisi. Vivyo hivyo, Sierra Leone ilikumbwa na vita vya kikatili kutokana na almasi — almasi zilizopewa jina la “blood diamonds” kwa sababu ziliigharimu nchi hiyo damu na machozi ya raia wake.

Kwa hivyo, ni lazima tuchukue tahadhari kabla ya kuchimba dhahabu ya Kakamega kwa kasi bila mipango. Serikali, viongozi wa eneo, na wananchi wanapaswa kuhakikisha kwamba madini haya yanachimbwa kwa uwazi, kwa kufuata sheria, na kwa manufaa ya wananchi. Kwanza kabisa, ushuru na mapato yatokanayo na madini haya lazima yawe na uwiano wa haki. Asilimia kubwa ya faida inapaswa kubaki kwa wananchi wa Kakamega kupitia miradi ya maendeleo kama vile shule, hospitali, barabara na maji safi.

Pili, fidia ya wale watakaohamishwa kutokana na shughuli za uchimbaji lazima iwe ya haki na ya haraka. Watu wasinyimwe ardhi zao au makazi yao bila mpango wa kuwasaidia upya. Aidha, serikali inapaswa kuhakikisha kuwa mazingira hayaharibiwi kwa sababu ya uchimbaji holela, kwani uchafuzi wa mito na udongo unaweza kuleta athari kubwa kwa wakulima na vizazi vijavyo.

Isitoshe, usalama wa wananchi lazima uimarishwe. Uchimbaji wa madini mara nyingi huvutia magenge ya kihalifu, walafi wa mali, na hata wanasiasa wasio waaminifu wanaotaka ujinufaisha binafsi. Ni jukumu la viongozi wa kitaifa na kaunti kuhakikisha kuwa wananchi wanalindwa, na kwamba mali ya nchi inatumika kwa ustawi wa wote, si wachache.

Kwa jumla, dhahabu ya Kakamega inaweza kuwa nguzo ya maendeleo ikiwa itasimamiwa kwa uadilifu, uwazi na hekima. Lakini ikiachwa mikononi mwa walafi na wageni wanaotafuta faida, inaweza kuwa chanzo cha migogoro, umasikini na uharibifu. Wakati ni huu wa kuhakikisha kuwa “madini yetu” yanakuwa baraka kwa Wakenya wote, si laana kwa vizazi vijavyo.

Tukijifunza kutoka historia ya DRC, Sierra Leone, na mataifa mengine, tunapaswa kujiuliza – je, tutaruhusu historia ijirudie? Jibu liko mikononi mwa viongozi wetu na raia wa Kakamega. Dhahabu ya Kakamega iwe dhahabu ya maendeleo, si dhahabu ya machozi.

LEAVE A REPLY