Mashirika ya kijamii na kidini yakishirikiana na Serikali ya Kaunti ya Mombasa yameendelea kutekeleza kampeni ya huruma kwa watu wa Palestina kupitia mpango unaoitwa “Panda Mti, Okoa Uhai.”
Lengo kuu la kampeni hii ni kukusanya shilingi milioni 30 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika zaidi ya 150,000 walioumia katika Ukanda wa Gaza, huku ripoti zikionyesha kuwa takribani watu 70,000 wamepoteza maisha kutokana na mapigano yanayoendelea.
Tarehe 7 Novemba, hafla ya uchangishaji fedha ilifanyika Mombasa na kufanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 15, na hivyo kufanya jumla ya michango kufikia milioni 25.
Siku iliyofuata, tarehe 8 Novemba, wananchi mamia walijitokeza kwa maandamano ya amani katika mama Ngina Waterfront kuonyesha mshikamano wao na wananchi wa Palestina.
Mwenyekiti wa Voices for Palestine, Ahmed Sharrif, amewahimiza watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuunga mkono juhudi hizi kwa kupanda miti na kuchangia misaada, akisema ni njia ya “kuokoa maisha na kulinda utu.”
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kususia bidhaa kutoka kwa makampuni yanayohusishwa na ufadhili wa vita hivyo
Tunaomba watu wote wenye nia njema wajitokeze kuunga mkono kampeni hii ya PLANT A TREE SAVE A LIFE
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Maimamu, Mohammed Dor, ameishukuru jamii kwa ushirikiano na kuwasihi wale waliotoa ahadi za michango kuzitimiza kwa wakati.

Kampeni hii pia imepanga kupanda miti 10,000 mwanzoni mwa mwaka 2026 kama kumbukumbu kwa wale waliopoteza maisha huko Gaza.



