Kamati Ya Bajeti Bunge la Kitaifa yaanza vikao vya Kuhakiki Na Kutathmini Bajeti Ya 2024/2025

0
156

Kamati Kuu ya Bajeti na Mgao wa Fedha katika Bunge la Kitaifa imeanza rasmi kikao chake maalum cha kuhakiki na kutathmini utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025. Kikao hicho cha siku kadhaa kinafanyika Mjini Mombasa, kikilenga kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya kuboresha utekelezaji wa bajeti ya kitaifa.

Akizungumza katika kikao cha kwanza, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Bungeni Samuel Atandi, ambaye pia ni Mbunge wa Alego Usonga, ameitaka Kamati hiyo kuchambua kwa kina matumizi ya fedha za umma na utekelezaji wa miradi iliyoidhinishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.

“Kamati hii ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa kila shilingi ya mlipa kodi inatumika kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria,” alisema Atandi.

Mdhibiti wa Bajeti wa Kitaifa, Dkt. Margaret Nyakang’o, aliwasilisha ripoti ya ofisi yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita, akibainisha kwamba baadhi ya wizara na idara za serikali zilishindwa kutekeleza miradi iliyopangiwa licha ya kupokea mgao kamili wa fedha.

Aidha, Dkt. Nyakang’o alieleza kuwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 ulishuhudia upungufu wa mikopo ya nje, huku mikopo ya ndani ikiongezeka ili kufidia mahitaji ya kifedha ya serikali.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Dkt. Kamau Thugge, pia alihudhuria kikao hicho na kutoa maelezo kuhusu changamoto zinazoathiri utekelezaji wa bajeti, ikiwemo ucheleweshaji wa mgao wa fedha kwa serikali za kaunti na baadhi ya idara za serikali kuu.

Kamati hiyo inatarajiwa kuendelea na vikao vyake siku ya Alhamisi na Ijumaa, ambapo Waziri wa Fedha Mhe. John Mbadi pamoja na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bi. Nancy Gathungu watafika mbele ya Kamati hiyo kutoa maelezo kuhusu bajeti ya mwaka uliopita na mipango ya mwaka wa fedha 2025/2026.

 

LEAVE A REPLY