Miaka ya sitini, Kenya na Singapore zilianza safari yao ya kujitawala kwa matumaini, ndoto, na matarajio sawa. Zote zilikuwa nchi changa, zenye rasilimali finyu lakini zenye nguvu kazi changamfu na ari ya kujijenga. Lakini leo hii, miaka zaidi ya sitini baadaye, Singapore ni taifa lililoendelea, la viwanda, teknolojia na nidhamu isiyotetereka. Kenya je? Je, sisi tumejifunza? Tumejipanga? Au tumeendelea kuwa na matumaini ya ajabu yasiyo na mwelekeo?
Singapore ilikumbatia nidhamu, uwajibikaji, na maono ya muda mrefu. Leo, ni kitovu cha biashara duniani, bandari zake ni miongoni mwa zinazotegemewa zaidi, elimu yao ni ya kiwango cha juu, na huduma kwa raia imejengwa kwa misingi ya ufanisi. Viongozi wake waliweka maslahi ya taifa mbele ya tamaa binafsi. Je, sisi hapa Kenya tunafanya hivyo?
Tuna ardhi yenye rutuba, vivutio vya kitalii vya kipekee, rasilimali za kila aina na watu werevu. Lakini kwa nini bado tunahangaika na matatizo yale yale ya miaka hamsini iliyopita – ufisadi, huduma duni, siasa za mgawanyiko na miundombinu inayosuasua? Je, ni laana au ni chaguo?
Singapore haikupata muujiza wa maendeleo. Haikubahatisha. Iliamua. Ilijipanga. Ilitekeleza. Na ikaendelea mbele. Kwa nini sisi hatuwezi? Tuna nini kinachotuzuia? Ni viongozi? Ni wananchi? Ni mfumo? Au ni ukosefu wa maamuzi ya kweli ya kuleta mabadiliko?
Kenya inaweza. Tunaweza. Lakini si kwa maneno matupu wala mipango ya maonyesho. Ni kwa vitendo vya dhati, maamuzi magumu, na kujitolea kwa pamoja. Tunahitaji kuwajibika, kuwa na nidhamu ya kitaifa na kuweka Kenya mbele ya matumbo yetu.
Je, hatuchoki kuwa taifa la ahadi zisizotimizwa? Je, hatufai kuwa taifa linalotazamwa kama mfano wa Afrika kama ambavyo Singapore ni mfano wa Asia? Ni wakati wa kuamka. Ni wakati wa kusema inatosha inatosha siasa za porojo, inatosha ufisadi, inatosha kupoteza muda.
Nitauliza kuwa iwapo singapore iliweza na ikasonga zaidi mbele, kwa nini sisi tusiweze?



