JE, IKULU IMEGEUKA CHUMBA CHA KAMPENI?
Katika siku za hivi karibuni, tumeona mfululizo wa mikutano mingi inayoandaliwa katika Ikulu ya Nairobi, ambayo imekuwa ikipewa majina mbalimbali kama ya “uwezeshaji”, “kuchochea maendeleo”, au “kuleta mageuzi”. Lakini chini ya pazia hilo, hali halisi ya mambo inaibua maswali makubwa: Je, Ikulu imegeuka jukwaa la kampeni za mapema kwa ajili ya uchaguzi wa 2027?
Kama raia, tuna haki ya kuuliza Je, mikutano hii ina manufaa gani ya moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida?
Ni jambo la kusikitisha kuona serikali ikitumia mabilioni ya fedha kuandaa mikutano, kulipia hoteli, kuweka mafuta magari ya viongozi, kulipa posho za maafisa, na gharama nyinginezo zisizo za lazima, huku maelfu ya Shule zikiwa bado hazijapokea fedha za msingi.
Wahadhiri wakidai malimbikizi ya mishahara ambayoi , imekawia kulipwa huku Sekta ya afya ikiyumba na Ajira kwa vijana ikiwa bado ni ndoto
Fedha hizi ambazo zinatumika kwa shughuli ambazo hjazieleweki manufaa yake zingesaidia kulipa madeni haya, kuinua elimu, au hata kutengeneza ajira mpya.
Katika makala haya , nimeuliza swali hili tena na tena Kama kweli miradi hii ni ya maana, mbona wanasiasa ndio wanasifia kuliko wananchi wa kawaida
Tumeshuhudia viongozi wa serikali na washirika wa kisiasa wa Rais wakizunguka nchi nzima wakisema eti haya ni “mageuzi ya kiuchumi”, lakini bila kuwepo kwa uthibitisho wa moja kwa moja wa mafanikio au mabadiliko yanayogusa maisha ya Mkenya wa kawaida. Ni kama miradi hii inajisifia yenyewe, badala ya kusifiwa na wale wanaofaidika nayo.
Nitasema hivi ikulu si jukwaa la siasa. Ni taasisi ya kitaifa inayopaswa kudumisha heshima, hadhi na kutopendelea upande wowote wa kisiasa. Ikiwa rais anaitumia kupanga mikutano ya mara kwa mara yenye sura ya kisiasa, huku akizungukwa na washirika wa kisiasa wanaoonekana wazi kuelekea 2027, basi hiyo ni kampeni ya mapema kwa kutumia rasilimali za umma jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utawala bora.
Wakati huu wa changamoto za kiuchumi ,Serikali inapaswa kutoa kipaumbele kwa huduma za msingi kama elimu, afya, na ustawi wa vijana.Mikutano ya kisiasa au ya “uwezeshaji” inayogharimu mabilioni ipaswe kuangaliwa upya.
Rais ahakikishe kuwa Ikulu inabaki kuwa taasisi ya kitaifa, si ya chama wala kampeni.



