Washington, MAREKANI
Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya kuanza mchakato wa kuiondoa Marekani kuwa mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Hili ni jambo kubwa,” rais mpya wa Marekani aliyeapishwa alisema alipokuwa akiidhinisha hati hiyo baada ya kurejea tena katika Ikulu ya Marekani.
Ilikuwa ni moja ya amri kadhaa za utendaji alizotia saini siku ya kwanza madarakani.
Hatahivyo uamuzi wake huenda sio tu ukaathiri utandekazi wa shirika hilo la Afya bali hata huduma zake kote duniani.
Kulingana na taarifa za matumizi ya fedha za hivi karibuni zilizotolewa na WHO, Marekani ndio mfadhili mkubwa wa shirika hilo .
Lakini Je, kwanini Trump ameamua kuchukua uamuzi huu?
Hii ni mara ya pili kwa Trump kuamuru Marekani kujiondoa kuwa mwanachama wa WHO.
Trump alikosoa jinsi shirika hilo la kimataifa lilivyoshughulikia janga la Covid-19 na kuanza mchakato wa kujiondoa kutoka kwa taasisi hiyo ya Geneva wakati wa janga hilo.
Rais Joe Biden baadaye alibatilisha uamuzi huo.
Agizo hilo lilisema Merekani inajiondoa “kwa sababu ya WHO kutoshughulikia janga la Covid-19 ambalo liliibuka Wuhan, China, na majanga mengine ya afya ya ulimwengu, kushindwa kwake kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka, na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa yasiyofaa. ushawishi wa kisiasa wa nchi wanachama wa WHO”.
Amri hiyo ya utendaji pia ilisema hatua hiyo ilitokana na “malipo yasiyofaa” ambayo Marekani ilitoa kwa WHO, ambayo ni sehemu ya Umoja wa Mataifa.
Trump alipokuwa ofisini kwa mara ya kwanza alikosoa shirika hilo kwa “kuipendelea China” katika kukabiliana na janga la Covid-19.
Aliishutumu WHO kwa kuegemea China kwa jinsi ilivyotoa mwongozo wakati wa mlipuko huo.
Mwaka 2020 wakati wa janga la Covid Tru
mp alisema: “Ikiwa WHO ingekuwa imefanya kazi yake ya kutuma wataalamu wa kitabibu nchini China ili kutathmini hali ilivyo, na kuikosoa China kwa kutokuwa wazi, ugonjwa huo ungeweza kudhibitiwa na kutokea kwa idadi ndogo ya vifo.”
WHO imekuwa ikifadhiliwa vipi?
Shirika hilo liliundwa 1948 kama sehemu ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, likilenga kuendeleza afya bora, kuhakikisha dunia inakuwa salama na kuhudumia wale walio katika hatari zaidi.”
Taasisi hiyo, ambayo makao yake makuu ni Geneva (Uswizi), imekuwa ikipata Ufadhili wa lazima na ule wa kujitolea
Kwanza, kuna pesa ambazo ni lazima zitolewe na nchi washirika 194.
Kila nchi inatakiwa kulipa kiwango fulani kulingana na Umoja wa Mataifa kupitia mfumo ambao ni vigumu kuelezeka kwasababu unazingatia utajiri wa nchi na idadi ya watu.
Ni pesa ambayo kwa msingi huwa inasimamia mishahara na utawala wa shirika hilo.
Pili ni ufadhili wa kujitolea unaowezesha nchi na maeneo kuahidi pesa watakazochangia kwa maswala maalum, kama vile chanjo ya ugonjwa wa polio, afya ya wanawake au ukabilianaji na matumizi ya tumbaku.
Marekani ilichangia dola za Marekani bilioni 1.284 katika kipindi cha 2022-2023, kuwezesha WHO, Marekani na nchi nyingine na washirika kutambua na kukabiliana na dharura, kuzuia vitisho vya magonjwa kuenea katika mipaka na kuendeleza vipaumbele vingine muhimu vya afya duniani.
WHO ilipokea dola za Marekani milioni 363 kama fedha za ufadhili kipindi cha 2022-2023 kulingana na taarifa katika wavuti wa shirika hilo.
Habari hii ni kwa hisani ya shhirika la BBC