Nairobi, KENYA
Mahakama Kuu jijini Nairobi imesimamisha makubaliano kati ya Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Kenya (KETRACO) na Adani Energy Solutions, ambayo ni kampuni ya India ya Adani Group.
Mkataba huo, uliotiwa saini Oktoba 11 na wenye thamani ya shilingi bilioni 95.68 unahusisha kampuni ya Adani kufadhili na kusambaza nguvu za umeme katika vituo vidogo kote nchini.
Hatua hiyo ya mahakama inafuatia ombi lililowasilishwa mahakamani na chama cha Wanasheria nchini (LSK) kutaka mkataba huo usitishwe hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Katika ombi hilo, lililoidhinishwa kuwa la dharura, LSK inasema makubaliano hayo yanakiuka katiba na yaliyofanywa kisiri bila kanuni zifaazo.
LSK inasema serikali haikushirikisha umma hivyo wananchi wana wasiwasi mkubwa kuhusu makubaliano hayo.
Katika uamuzi wake Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alisema ombi la LSK liliafikia kiwango cha kisheria kinachohitajia kwa mahakama kutoa maagizo ya kusimamisha makubaliano ya kampuni za KETRACO-Adani.