Nairobi, KENYA
Wakili wa Rais William Ruto ameambia mahakama kuu kwamba anamwakilisha mteja wake aliyesema Mahakama kuu ya Kenya haina mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi zilizowasilishwa kupinga kumuondoa Rigathi Gachagua madarakani.
Jopo la majaji watatu Eric Ogola, Anthony Mrima na Freda Mugambi lilichanguliwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kusikiliza kesi zote zinazopinga mchakato wa kumuondoa Rigathi Gachagua madarakani.
Kupitia Wakili Adrian Kamotho, Ruto anadai kuwa Mahakama ya Juu Zaidi pekee ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.
Kulingana na Rais William Ruto, mahakama kuu inafaa kutupilia mbali kesi hizo akidai kuwa zimewasilishwa kinyume cha sheria na ni utumiaji mbaya wa mchakato wa mahakama.
Rais Ruto ameongeza kuwa kesi dhidi ya Rais au mtu anayetekeleza majukumu ya afisi ya Rais katika kipindi cha uongozi wake kuhusiana na jambo lolote lililofanywa au kutofanywa chini ya sheria ya Katiba ya Kenya 2010 haziwezi kufunguliwa katika mahakama yoyote tu.
Siku ya Jumanne Oktoba 22, 2024 kulishuhudiwa majibizano makali kutoka kwa mawakili wa upande wa Gachagua na wale wanaotetea hatua ya kumuondoa Gachagua afisini huku mawakili wa Gachagua wakihoji uhalali wa naibu jaji mkuu kuteua jopo la majaji hao watatu kusikiliza kesi hiyo.