Nairobi, KENYA
Mahakama kuu imesitisha kwa muda hatua ya bunge la Seneti kuidhinisha mashtaka ya kumuondoa madarakani Rigathi Gachagua.
Uamuzi huo umetolewa muda mfupi tu baada ya Bunge la Kitaifa kukubali uteuzi wa Kithure Kindiki kuwa Naibu wa Rais baada ya Rais William Ruto kuwasilisha jina lake kwenye bunge hilo.
Hapo jana Maseneta waliidhinisha mashtaka 5 kati ya 11 dhidi ya Gachagua na kumuondoa ofisini.
Gachagua alikosa kufika mbele ya maseneta kujitetea baada ya mawakili wake kusema alipatwa na ”maumivu makali ya kifua” na kulazimika kulazwa hospitalini.
Uamuzi uliotolewa na Jaji Chacha Mwita umezuia kutekeleza azimio hilo la seneti na pia kuzuia rais kumteua mtu kuichukua nafasi hiyo hadi tarehe 24 mwezi huu wakati kesi hiyo itakaposikilizwa na jopo la majaji watakaoteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Hata hivyo tayari rais amependekeza jina la Kithure Kindiki kuichukua nafasi ya Gachagua na bunge la taifa kukubali uteuzi wake.