Naibu Wa Rais Rigathi Gachagua Augua Ghafla Na Kulazwa Hospitalini, Bunge La Seneti Likiendelea Na Kikao

0
93
Rigathi Gachagua akiwa mbele ya bunge la Seneti

Nairobi, KENYA

Naibu rais Rigathi Gachagua amelazwa hospitalini baada ya kuugua ghafla wakati kesi kuhusu hoja ya kumuondoa mamlakani ilipokuwa ikiendelea katika bunge la Seneti.

Wakili wa Gachagua ameambia bunge hilo kuwa mteja wake amepatwa na matatizo ya kifua na ikabidi apelekwe hospitali.

Gachagua alitarajiwa kujitetea mbele ya Bunge hilo la Seneti dhidi ya madai yanayomkabili lakini hakufika bungeni kabla ya wakili wake kuelezea kuwa alikumbwa na matatizo ya kiafya.

Hata hivyo, Bunge hilo limepiga kura kuendelea na hoja ya kumuondoa madarakani Rigathi Gachagua bila ya yeye kuwa mbele ya bunge la Seneti.

“Kwa vile mchakato huu unaendana na muda kulingana na katiba, na ikizingatiwa kuwa muda unakamilika Jumamosi, fursa pekee iliyopo ni kutangaza Jumamosi kama siku ya mwisho ya kusikiliza hoja hii,” Kingi alielekeza Bunge kabla ya maseneta hao kupiga kura.

Na baada ya hapo, maseneta walipiga kura ya kiutaratibu ya iwapo wakubali au wakatae kuendelea na hoja ya kuahirisha kikao hadi tarehe nyingine ambayo ilikuwa imependekezwa na Spika wa Bunge Amason Kingi.

Lakini baada ya kuulizwa swali la  kukubali au kukataa, Bunge lilikataa kusongeza mbele tarehe ya kusikiliza hoja ya kumuondoa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Baada ya Bunge kuamua kuendelea na kikao cha kujadili hoja hiyo, mawakili wanaomwakilisha Naibu Rais Rigathi Gachagua walitoka nje ya Bunge.

“Kutokana na uamuzi wa Seneti, sisi kama timu ya wanasheria wanaomwakilisha naibu rais hatuwezi kuendelea kuwepo Bungeni bila maagizo. Kwa hivyo tunaondoka,” alisema Wakili Mkuu Paul Muite, anayemwakilisha Gachagua.

Hiatua hii iliwadia baada ya wakili wa Rigathi Gachagua Paul Muite, kusema kuwa naibu rais hataweza kufika mbele ya Bunge leo kwasababu anaugua maumivu makali ya kifua.

LEAVE A REPLY