Bunge La Seneti Lasikiliza Kesi Ya Kumuondoa Rigathi Gachagua

0
91
Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua

Nairobi, KENYA

Bunge la Seneti nchini Kenya limeanza hatua ya mwisho ya kusikiliza kesi ya mchakato wa kutaka kumuondoa mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Wiki iliyopita wabunge walipiga kura katika Bunge la Kitaifa kuidhinisha hoja ya kumuondoa madarakani, na hivyo kuweka mazingira ya kusikiliza kesi kwa siku mbili katika Seneti ambayo itaamua iwapo atamtimua au la.

Naibu Rais anakabiliwa na mashtaka 11 yakiwemo ufisadi, kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu serikali – yote anayakana.

Mchakato huo unafuatia mzozo wake wa hivi majuzi na Rais William Ruto, ambaye amekuwa kimya kuhusu suala hilo.

Kesi ya Gachagua inaendeshwa mbele ya bunge zima la Seneti baada ya kukataa mchakato wa kuunda kamati ya watu 11 kuchunguza mashtaka hayo.

Kesi hiyo ilianza Jumatano asubuhi na baada ya vikao vya awali, mashtaka yalisomwa kwa naibu rais.

Siku ya Alhamisi, kesi itaendelea kushughulikia ushahidi na mashahidi kutoka upande wa Gachagua hadi alasiri.

Mwishoni mwa mchakato huo jioni, maseneta watajadili hoja hiyo kwa takriban saa mbili na kisha kupiga kura – iliyopangwa kufanyika Alhamisi kuanzia saa mbili usiku.

Thuluthi mbili ya wajumbe 67 wa Seneti lazima waidhinishe hoja hiyo ili kumuondoa  Gachagua afisini.

Iwapo hilo litatimia basi Gachagua hataweza kushika wadhifa wowote wa umma tena.

Anatarajiwa kupinga mashtaka hayo katika mahakama iwapo yataidhinishwa na bunge la Seneti.

LEAVE A REPLY