
Nairobi, KENYA
Kenya itatuma maafisa 600 zaidi wa polisi nchini Haiti mwezi ujao kuunga mkono mpango wa kimataifa wa kuimarisha usalama nchini humo.
Rais William Ruto amedokeza hayo alipohutubia wanahabari alipomkaribisha waziri mkuu wa Haiti Garry Conille katika ziara iliyonuiwa kuharakisha kutuma jeshi hilo.
Mataifa 10 yameahidi kutuma jumla ya wanajeshi 2,900 kusaidia kuimarisha Usalama, mpangoi unaoongozwa na Kenya.
Lakini ni maafisa 430 pekee waliotumwa tangu ujumbe huo ulipoidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwezi Juni, 400 kati yao kutoka Kenya.
Magenge yenye silaha kali, ambayo yanadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Port-au-Prince, yameendelea kudhibiti eneo hilo.
Wiki iliyopita, wanachama wa genge la Gran Grif walifanya moja ya mashambulizi mabaya zaidi nchini humo katika miaka ya hivi karibuni, na kuua watu wasiopungua 115.
Rais Ruto aliwaambia wanahabari kuwa misheni hiyo inaboresha usalama nchini Haiti, akitaja vita dhidi ya magenge “vita ambavyo tunaweza kushinda”.
Alisema maafisa 600 wa ziada tayari wanapitia mafunzo na watakuwa tayari kwa kazi mwezi ujao.
Waziri Mkuu wa Haiti, Garry Conille, alisifu namna polisi wa Kenya walivyojibu mashambulizi yaliyosababisa mauaji wiki jana.
“Polisi na kikosi (cha Kenya) kilishika doria ipasavyo barabarani na kwa kweli, karibu kwa saa moja – ili kuhakikisha kuwa jiji linalohusika linalindwa” Conille alisema.
Kulingana na umoja wa mataifa, Zaidi ya watu elfu 700 nchini Haiti wamekimbia makazi yao na zaidi ya milioni tano wanakabiliwa na njaa, hii ikiwa ni karibu nusu ya idadi ya watu nchini Haiti.