‘Kufa Makanga, Kufa Dereva’: Wakenya Wachoshwa Na Utawala Wa Rais William Ruto

0
78
Wakenya eneo la Nyeri Oktoba 4, 2024 wakilalamikia uongozi m-baya (Picha - Standard)

Nairobi, KENYA

Idadi kubwa ya wakenya waliojitokeza kutoa maoni kuhusu hoja ya kumuondoa mamlakani naibu rais Rigathi Gachagua walibadilisha kauli na kukashifu utawala wa Rais William Ruto wakati wa zoezi hilo la Ijumaa na Jumamosi nchini Kenya.

Kauli hii “Kufa Makanga Kufa Makanga”iliyomaanisha rais na naibu wake wanapaswa kuondoka mamlakani inaonekana kama kifungua macho kwa rais anayejitahidi kujinasua kutoka kwa maandamano ya hivi majuzi ya vijana wa Gen Z yaliyoitikisa serikali ya Kenya Kwanza.

Hakuna kinachoonekana kuvutia wananchi katika serikali ya rais Ruto.

Sekta ya afya inayumba kufuatia mpango tata wa bima ya afya “SHA” unaowaacha Wakenya na wasiwasi.

Elimu ya juu ni mkanganyiko, huku mpango mpya wa kulipia karo na ufadhili wa masomo ya elimu ya juu ukipingwa na mahakama.

Mvutano pia unashuhudiwa katika pendekezo la kusimamia  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, ambao kwa muda mrefu umekuwa siri na serikali.

Sekta ya kawi nayo haikosi hitilafu zake huku nguvu za umeme zikikatika mara kwa mara.

Wakati bei ya unga ikionekana kupungua katika miezi ya hivi karibuni, hisia za wananchi ni kuwa gharama ya maisha bado iko juu.

Ukosefu wa ajira unashuhudiwa miongoni mwa vijana, huku serikali ikitafuta suluhu zisizoelewekwa kwa wananchi kama vile kusafirisha vijana nje ya nchi ili kufanya kazi.

Pamoja na hayo yote, viongozi wa kisiasa wamejitenga na ukweli na wanasukuma masuala ambayo Wakenya wanasema hayawahusu, kama vile hoja ya kutaka kumuondoa mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Kupitia msukumo huo, wananchi wanaonekana kuona mwanya wa kuwaondoa Rais na makamu wake na kusukuma kauli ya Kufa makanga, kufa dereva.

Hayo yakijiri kuna pendekezo la Seneta wa Nandi Samson Cherargei la kutaka kuongeza muhula wa rais wa kuhudumu, kutoka miaka mitano hadi saba.

Wakenya walionekana kuchoshwa na namna serikali inavyoendeshwa wakati wa zoezi la kutoa maoni kuhusu naibu wa rais.

Matamshi ya mkenya Caroline Cheptoo, aliyewasuta wanasiasa katika ukumbi wa Bomas of Kenya, kwa mfano, yanadhihirisha hali ya wakenya wengi na serikali ya rais William Ruto.

“At least hata leo mmetukumbuka. Hamtuitangi hizi vitu, anyway. Leo mmekumbuka vijana na wananchi kwa sababu mna shida zenu. Nyinyi kutuita hapa ni wazi kwamba masuala yaliyoibuliwa na Gen Z na millenials m-meyapuuza kwa kushirikiana na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.” Caroline Cheptoo alifokea kwa ukali, viongozi waliokuwa katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.

LEAVE A REPLY