
Kinshasa, DRC
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kitovu cha ugonjwa wa Mpox, imeanza kampeni ya chanjo dhidi ya virusi hivyo.
Chanjo hizo zilianza kutolewa Jumamosi Oktoba 5, 2024, siku tatu baada ya tarehe iliyopangwa.
Chanjo hizo ilipangwa zianze kutolewa siku ya Jumatano kote nchini Kongo lakini mamlaka za afya ziliarifu kusitisha kabla ya waziri wa Afya wa Kongo, Samuel-Roger Kamba kutoa tarehe rasmi kuwa ni Jumamosi ya Oktoba 5.
Waziri Samuel-Roger Kamba amesema lengo la kampeni hiyo ni kuchanja watu walio katika hatari zaidi wakiwemo wahudumu wa afya.
“Tunazindua, siku ya Jumamosi, Okotba 5 kampeni ya utoaji chanjo,” alisema Kamba alipozungumza na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Kongo, Kinshasa.
Kampeni hiyo ya chanjo ilianzia kwenye mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini wa Goma uliopo mashariki wa Kongo, eneo ambalo limeathiriwa zaidi na maradhi ya Mpox.
“Chanjo ambayo Kongo inayo hivi sasa inatosha kuanza kuzitoa kwenye maeneo yaliyoathiriwa zaidi, lakini bado tunasubiri chanjo zaidi. “ alisema waziri Kamba
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Kongo imerekodi visa elfu 30 vya Mpox, na vifo vya watu 988.
Kwa mujibu wa waziri wa afya, asilimia 70 ya vifo hivyo ni vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano, na kuongeza kwamba watoto ndio walioathiriwa zaidi na virusi hivyo.
Hata hivyo chanjo zilizopo hivi sasa nchini Kongo zinazotengenezwa na kampuni ya Denmark ya Bavarian Nordic ni kwa ajili ya watu wazima pekee.