Goma, DRC
Zaidi ya watu 70 wamefariki baada ya meli kuzama kwenye ziwa kivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Watu kadhaa bado hawajulikani walipo katika mkasa huo mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo linalokabiliwa na miundombinu duni.
Taarifa zinasema meli hiyo iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 150 na mizigo ilizama muda mfupi kabla ya kuwasili katika bandari ya mjini Goma.
Ilikuwa inatoka kwenye mji wa Minova katika jimbo jirani la kivu kusini .
Kulingana na vyanzo vya ndani , meli hiyo kwa jina Merdy, ilizama Ijumaa kabla ya saa nne asubuhi kwenye ziwa Kivu karibu mita 200 na soko kuu la Kituku .
Watu wachache walionusurika wamefikishwa mjini Goma wakiwa katika hali mahututi na wengine walifariki muda mchate tu baada ya kufikishwa nchi kavu.
Mbali na abiria waliokuwemo, meli hiyo pia ilikuwa imebeba shehena ya chakula na vifaa vingine muhimu kutoka katika mji mdogo wa Minova jimboni kivu kusini.
Ziwa kivu, ndilo limesalia kuwa njia pekee inayotumiwa kusafirisha bidhaa kwenda katika mji wa Goma, tangu barabara ya kuelekea huko ifungwe na wapiganaji wa kundi la M23 miezi michache iliyopita .
Raia waliofika hapa kutafuta miili ya wapendwa wao wameelezea kusikitishwa na kile wanacho taja kama uzembe wa serikali hasa katika suala la miundombinu.
Polisi hata hivyo , imeendelea na zoezi la kutafuta abiria zaidi waliokuwa kwenye meli hiyo.