Nairobi, KENYA
Bunge la Kitaifa limeongeza siku moja zaidi ya zoezi linaloendelea la kukusanya maoni ya umma kuhusu hoja ya kutaka kumuondoa mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Zoezi hilo lililoanza Ijumaa Oktoba 10, 2024 sasa litaendelea hadi Jumamosi Oktoba 11 ili kuruhusu Wakenya kuwasilisha maoni yao kuhusu suala hilo.
Katika notisi iliyotolewa Ijumaa, Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge alisema siku moja zaidi ya kutoa maoni imeongezwa kufuatia agizo la Mahakama Kuu.
Njoroge amesema nyongeza hiyo itawapa wakenya muda wa kutosha kuwasilisha maoni yao katika maeneo bunge yote 290.
Mahakama kuu Alhamisi iliamuru Bunge kufanya awamu ya pili ya kukusanya maoni ya umma ili kuhakikisha Wakenya wote wanashiriki zoezi hilo.
Jaji Richard Mwongo wa Mahakama ya Sheria ya Kerugoya aliona kwamba hatua ya kushirikisha umma lazima ihusishe maoni ya Wakenya wote .
Alieleza kuwa mchakato huo lazima uwe wazi ili wananchi waelewe.
Zoezi hilo lilianza Ijumaa, licha ya Naibu rais Rigathi Gachagua kuelekea Mahakamani kujaribu kuzuia zoezi hilo.
Kulingana na Katiba, Bunge la Kitaifa lina ratiba ya siku saba, ambayo itakamilika Jumanne, ili kuamua kuhusu hoja maalum ya kumuondoa Gachagua mamlakani kabla ya bunge la Seneti kuamua kuhusu suala hilo.