Geneva, SWITZERLAND
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya (WHO) linasema ingawa Afrika ina barabara na magari machache zaidi kuliko kanda zingine, ndiyo yenye idadi kubwa kabisa ya vifo vya ajali za barabarani.
Ripoti ya WHO inasema ajali hizo zinachochewa na uzembe wa madereva, mwendo wa kasi, ulevi, miundo mbinu duni na magari mabovu.
Barani Afrika, ambako vifo 620 vya barabarani hutokea kila siku, hali huwa ni mbaya zaidi kutokana na barabara mbaya, magari makuukuu na upungufu wa huduma za dharura.
Ripoti hiyo ya WHO inasema Afrika imelitangulia eneo la kusini mashariki mwa Asia kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vya barabarani .
Mwaka uliopita, Afrika – yenye asilimia 4 tu ya magari yote ulimwenguni – ilikabiliwa na asilimia 19 ya vifo vilivyotokana na ajali za barabarani ulimwenguni.