Nairobi, KENYA
Spika wa bunge la kitaifa la Kenya Moses Wetangula ameidhinisha hoja ya kumuondoa afisini Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Wetangula amesema sababu zote 11 zilizoorodheshwa za kushinikiza hoja hiyo, zinaambatana na katiba.
Hoja hiyo imewasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Mutuse anasema wabunge 291 tayari wametia saini ombi la kumwondoa naibu huyo wa rais afisini.
Wabunge waanaounga mkono juhudi hizo wanamshutumu Rigathi Gachagua kwa kuhusika katika maandamano ya kupinga serikali mwezi Juni,kuhusika katika ufisadi, kuhujumu serikali na kuendeleza siasa za mgawanyiko wa kikabila.
Naibu rais hata hivyo anapuuza madai hayo.
Katika siku za hivi karibuni, tofauti kubwa zimeshuhudiwa baina ya rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua huku wabunge wanaoegemea upande wa rais na wale wa naibu wake wakirushiana maneno hadharani.
Hoja ya kutaka kumuondoa mamlakani naibu rais Rigathi Gachagua inaonekana kama kilele cha mzozo huo mkubwa kati ya Gachagua na Rais William Ruto.
Juhudi za awali za naibu rais Rigathi Gachagua kutaka kusitisha jaribio la kumuondoa madarakani kupitia mahakama ziliambulia patupu.
Mzozo wa mamlaka kati ya rais na naibu wake umesababisha wasiwasi serikalini wakati ambapo Kenya ikipambana kujikwamua kiuchumi.
Ruto alimchagua Gachagua kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa 2022, alipomshinda aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
Gachagua anatoka katika eneo la Mlima Kenya lenye kura nyingi, na anasema alikuwa na mchango mkubwa kwa ushindi wa rais Ruto.