Wanafunzi Waelimishwa Mjini Mombasa Ili Kukabiliana Na Uhalifu Wa Mtandaoni

0
213
Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya usalama wa mtandaoni yaliyofanyika mjini Mombasa. (Picha: Shem Oburu)

Mombasa, Kenya

Zaidi ya vijana 500 walio na ujuzi wa teknolojia ya mtandao kutoka taasisi mbalimbali pwani ya Kenya wamenufaika na mafunzo maalum kuhusu usalama wa mtandao yaliyofanyika mjini Mombasa.

Mafunzo hayo yameandaliwa na mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya (CA) kwa ushirikiano na kampuni ya Huawei na muungano wa kuangazia usalama wa mtandaoni, Kenya CyberSecurity and Forensics Association (KCSFA).

Mafunzo hayo yaliambatana na mashindano kuhusu usalama wa mtandaoni ya Cybersecurity Bootcamp na Hackathon ili kuhusisha vijana katika harakati za kubadilisha taifa kidijitali.

Boot Camp ni programu yenye ushindani wa hali ya juu ya kujifunza maswala mengi mtandaoni.

Kwa kawaida Boot Camp hulenga kutoa ujuzi na maarifa ya kimsingi kuhusu usalama mtandaoni kwa wanafunzi wanaoendelea na elimu katika vyuo, vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi.

Naibu Mkurugenzi wa CA anayehusika na masuala ya Usalama wa Mtandao Dkt Vincent Ngundi anasema mashindano ya hackathon ni mfululizo wa mafunzo ya Usalama wa mtandaoni yanayolenga kuwapa ujuzi zaidi wataalamu wa usalama wa mtandao ambao wana jukumu la kulinda mamilioni ya wakenya wanaotumia mtandao.

“Lengo letu ni kuhakikisha ujuzi wa masuala ya mtandao unapiga hatua na tuweze kukabiliana na mashambulio mtandaoni yanayoongezeka kwa kasi, na yakiwa ya kisasa zaidi kumaanisha tunafaa kujiimarisha.” alisema Dkt Ngundi akiwa mjini Mombasa wakati wa hafla ya kutuza vijana walioshinda mashindano ya hackathon.

Washindi wa Bootcamp walikuwa Hezbon Vincent, Erick Mwangi, na Esther Muthoga, Elias Omondi, Felix Muriithi, na Nicholas Mwangi, wakati washindi wa Bootcamp wakiwa Lenox Akhonya, Zainab Juma, na Sherry Obare.

Kwa mashindano ya Hackathon, vijana wa THEE GOATS waliibuka washindi na watawakilisha Mombasa katika mashindano ya kitaifa mwezi Oktoba. Vijana wa APT 1337 waliibuka wa pili huku vijana wa BE-HACKERS wakimaliza wa tatu.

Mashindano haya yamekuwa yakiendelea na tayari yamefanyika kaunti za Nyeri, Kisumu, Eldoret, na Mombasa,  kilele chake kitakuwa Oktoba 2023 kuangazia Zaidi  usalama mtandaoni yaani October Cyber Security Awareness Month (OCSAM).

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA) inaelezea umuhimu wa kuwezesha na kuwapa ujuzi zaidi wataalam katika masuala ya mtandao ili kulinda watumiaji milioni 11 wa mitandao ya kijamii nchini dhidi ya uhalifu wa mtandaoni.

CA imeeleza kuwa idadi ya mashambulio ya mtandaoni imeongezeka hadi milioni 860 kutoka milioni 7.7 katika muda wa miaka mitano, na kuiweka Kenya pamoja na Afrika Kusini na Nigeria miongoni mwa mataifa matatu barani Afrika yanayolengwa zaidi na mashambulio mtandaoni.

 

LEAVE A REPLY