
Mombasa, Kenya
Shule ya upili ya wavulana Allidina Visram imepanga msururu wa hafla maalum za sherehe, kuadhimisha miaka 100 tangu ianzishwe.
Shule ya Allidina Visram ni ya kutwa na iko katika barabara ya Abdell Nasser, eneo la Mvita kaunti ya Mombasa.
Ilianzishwa mnamo mwaka 1923 na ni miongoni mwa shule zilizojizolea sifa nyingi kwa kuandikisha msururu wa matokeo bora katika mitihani ya kitaifa.
Wakurugenzi wa shule hiyo wamesema lengo kuu la sherehe hizo ni kuleta pamoja wanafunzi wa zamani wa shule hiyo na washikadau mbalimbali kutoka sekta ya elimu.
Wanasema wanalenga kujenga upya shule hiyo na kuweka mazingira mazuri ya masomo ya kisasa, ikiwa ni pamoja na masomo ya kidijitali yaani digital learning.
Sherehe hizo za kihistoria zitahusisha mpango wa kusaidia jamii kama vile kusafisha sehemu kadhaa za jiji la Mombasa na pia mchango wa kutoa damu.
Hii ni njia moja ya shule hiyo kutoa mchango kwa jamii na kusaidia katika kuboresha maisha ya watu wanaowazunguka.
Sherehe hizo za kuadhimisha miaka 100 zitaanza rasmi Septemba 11, 2023 na kuendelea hadi Septemba 16, 2023.
Wasimamisi wa Allidina Visram wanasema hiyo itakua fursa ya kipekee ya kuimarisha uhusiano kati ya wadau wa shule na jamii, pamoja na kuthibitisha dhamira ya shule hiyo katika kutoa elimu bora na kusaidia maendeleo ya kisasa katika mafunzo.