Afariki Baada Ya Kuzirai Wakati Wa Majaribio Ya Kujiunga Na KDF Mjini Kilifi

0
202
Harrison Kazungu, aliyeaga dunia wakati wa majaribio ya kujiunga na KDF mjini Kilifi

Kilifi, Kenya

Mwanamume wa umri wa miaka 21 amefariki dunia baada ya kuzirai wakati wa majaribio ya vijana kujiunga na jeshi la KDF katika uwanja Karisa Maitha mjini Kilifi.

Harrison Kazungu Maitha, kutoka kijiji cha Ufuoni wadi ya Matsangoni kaunti ya Kilifi alizirai wakati wa majaribio ya kukimbia Septemba 5, 2023.

John Masha Maitha ambaye ni babake marehemu anasema mwanae alitoka nyumbani asubuhi akiwa na matumaini ya kuafikia ndoto yake ya kuwa jeshi wa Kenya.

John ameambia waandishi wa habari kwamba walishtushwa na  taarifa kuwa mwanao alilazwa hospitali ya rufaa ya Kilifi akiwa hali mahututi.

Ameongeza kuwa mtoto wake hakuwa na matatizo yeyote ya afya ila kulingana na ripoti ya daktari, alikosa hewa ya kutosha kwenye ubongo wake na hivyo ubongo ukasita kufanya kazi.

“Kijana wangu Harrison alikuwa ametamani ile kazi kwa muda, jumanne ya tarehe tano akarauka saa kumi kuelekea Kilifi  kujaribu bahati yake nikingoja jioni nipate majibu kama amefaulu au hajafaulu. Majira ya mchana nilipata taarifa kuwa alipokuwa katika mbio alianguka akapoteza fahamu na hata wakati huo alikuwa hospitali katika chumba cha huduma za dharura. Aliendelea kutibiwa madaktari wakamfanyia uchunguzi hadi Jumatano asubuhi walipobaini kuwa hewa ya oksijeni ilichelewa kufika katika ubongo wake na hakukuwa na njia yoyote m-badala ya kufufua ubongo wake.” Alisema John Masha Maitha, babake marehemu Harrison.

Mwili wa Harrison unahifadhiwa katika makafani ya hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kilifi.

Haya yamejiri siku moja tu baada ya tukio lingine sawia na hilo kutokea eneo la Gichugu kaunti ya Kirinyaga wakati mwanamume alipozirai akishiriki zoezi la kujiunga jeshini na baadaye kuaga dunia alipokuwa akitibiwa katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya.

LEAVE A REPLY