
Bungoma, Kenya
Rais William Ruto amesema serikali ishaamua kutatua changamoto zinazokumba kampuni za sukari nchini.
Rais amesema serikali itatatua suala hilo mara moja licha ya kwamba mageuzi yaliyotarajiwa katika sekta hiyo yalicheleweshwa.
“Tutaondoa wakiritimba ambao wanadai kudhibiti sekta ya sukari nchini.” Alisema Rais mjini Bungoma wakati wa ibaada ya maombi ya madhehebu mbalimbali.
Rais pia alibaini kuwa Serikali ina nia ya kufufua kilimo cha miwa Magharibi mwa Kenya kwa lengo la kubuni nafasi Zaidi za ajira na kupanua fursa za kiuchumi za vijana katika kanda hii.
Aliwataka viongozi kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kufanya kazi pamoja katika kubadilisha nchi kwa manufaa ya Wakenya.
Waliohudhuria ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Magavana Ken Lusaka (Bungoma), Fernandes Barasa (Kakamega), Paul Otuoma (Busia) na Wilber Ottichilo (Vihiga) na wabunge kadhaa.
Naibu rais Rigathi Gachagua naye alisema Utawala wa Kenya Kwanza uko mbioni kutimiza ahadi zake kama vile kubuni nafasi za ajira na kuongeza uzalishaji wa chakula.
“Hatuna shaka hata kidogo kwamba tutaipeleka Kenya mahali inapofaa kuwa,” alileza Rigathi Gachagua.