Seneta Cherargei Ataka Waziri Ababu Namwamba Ahojiwe Kwa Madai Ya Kunyanyasa Wanariadha

0
140
Seneta wa Nandi Samson Cherargei (Picha: Maktaba)

Seneta wa Nandi Samson Cherargei anaunga mkono kauli ya kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichungwa ya kutaka waziri wa michezo kufika mbele ya bunge la kitaifa kujibu maswali kuhusu unyanyasaji wa wanariadha wa Kenya.

Cherargei anasema maofisa wa wizara ya michezo wanatumia vibaya mamlaka kani hata husafiri na wapenzi wao wakiwaweka kama wawakilishi wa michezo.

Kupitia mtandao wake wa X Seneta huyo amesema anatathmini jinsi maofisa wa wizara hiyo wanasafiri pamoja na wapenzi wao katika nafasi za ngazi ya juu kwenye ndege ilhali wanariadha  wakiwachwa katika viti vya kawaida katika safari za michezo za Hungary na Budapest.

Ameongeza kuwa wachezaji wa kike wananyanyaswa kimapenzi na kiuchumi na kusisitiza kuwa waziri wa michezo Ababu Namwamba lazima afike mbele ya bunge kujibu maswala kuhusu sakata hiyo.

Katika kikao bungeni Ichungwa ameonesha kughadhabishwa na jinsi wizara ya michezo inavyonyanyasa wanariadha  kwani hata wakirejea nchini na matokeo mazuri, hakuna afisa wa michezo anayewapokea katika uwanja wa ndege.

Ameongeza kuwa waziri huyo ameshindwa kuwahudumia wanariadha  wa taifa la Kenya badala yake anafanya mzaha katika ofisi na kusisitiza kuwa waziri huyo lazima afike mbele ya bunge hilo la kitaifa ili kujibu maswali.

Hii si mara ya Kwanza kwa kisa kama hiki kushuhudiwa katika wizara ya Michezo, mwaka wa 2016 baada ya michezo ya Olimpiki mjini Rio nchini Brazil ambapo Kenya ilipata matokeo mema, ilibainika kuwa ufisadi ulikithiri katika sekta hiyo.

Aliyekuwa waziri wa michezo Hassan Wario  alishtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani au kulipa faini ya shilingi milioni 3.6 huku Stephen Soi akihukumiwa miaka 17 gerezani mwaka wa 2021 kwa tuhuma za ufisadi na unyanyasaji wa wanariadha kuanzia safari yao kutoka humu nchini hadi jinsi walivyoshughulikiwa nchini brazil.

Hukumu hizo hata hivyo zilibadilishwa na mahakama kuu kufuatia rufaa zilizowasilishwa na wakabaki huru.

LEAVE A REPLY