Kilifi, Kenya
Kifafa ni ugonjwa sugu wa ubongo unaofanya mtu kupata mshtuko katika ubongo na kusababisha mtu kuanguka na kuzirai.
Shirika la Afya Duniani, WHO linaeleza kuwa Kifafa ni mojawapo ya hali kongwe zaidi duniani inayotambulika.
Kaunti ya Kilifi imetajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa idadi kubwa ya watu wanaougua maradhi haya ya kifafa nchini Kenya.
Kamati ya kitaifa ya kushughulikia maradhi ya kifafa inasema kaunti ya Kilifi pekee ina zaidi ya wagonjwa elfu 10 wanaougua kifafa.
Katibu wa kamati hiyo Fredrick Beuchi ambaye pia ni mwanaharakati wa maradhi hayo, amedokeza kuwa Kilifi ina masuala mengi ambayo yamekuwa yakichangia ongezeko la maradhi hayo.
“Kenya watu zaidi ya milioni 1.5 wanaugua aina mojawapo ya hali hii ya kifafa, kuna sehemu zimeonekana kuwa na athari kubwa zaidi kutokana na masuala yanayochangia. Moja ya sehemu hii ni kaunti ya Kilifi. Kwa sasa watu zaidi ya elfu 10 wako na hali hii ya kifafa kaunti hii.” Alisema Fredrick Beuchi
Beuchi amesema huenda idadi hiyo ikaongezeka hata zaidi, iwapo wataalamu wa maradhi hayo wataendeleza shughuli za utafiti kwa wakenya katika maeneo mbali mbali nchini.
Haya yanajiri huku tafiti zikibaini kuwa takriban wakenya milioni 1.5 wanaugua maradhi ya kifafa.
“Tafiti nyingi sana za hali ya kifafa zimefanywa hii sehemu kwa sababu ya zile ambazo tunaita pre disposing factors ambazo zinafanya mtu kupata hali hii ya kifafa. Takwimu hizi ni za muda kwa hivyo kuna uwezekano ya kwamba kukifanywa takwimu zengine zozote zile basi watu huenda wakaongezeka na pia juhudi za kufanya tafiti zinaendelea.” Beuchi Aliongeza.
Ulimwenguni, kila mwaka takriban watu milioni 5 hugunduliwa kuwa na kifafa.
Katika nchi zenye kipato cha juu, inakadiriwa kuwa watu 49 kati ya elfu 100 wanagunduliwa kuwa na kifafa kila mwaka.
Katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, takwimu hii inaeleza kuwa watu 139 kwa kila watu elfu 100 hupatikana na ugonjwa huo kila mwaka.