Gavana Susan Kihika Amtaka Raila Anyamaze Na Kustaafu Siasa

0
169
Susan Kihika (kushoto) na Balozi wa Marekani Meg Whitman (kulia) katika mkutano wa ugatuzi mjini Eldoret.

Eldoret, Kenya

Gavana wa Nakuru Susan Kihika amemkosoa kiongozi wa ODM Raila Odinga kutokana na matamshi yake ya kumtaka balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman aepuke kujishughulisha na masuala ya taifa la Kenya.

Raila alitoa matamshi hayo Alhamisi Agosti 17, alipohutubia kongamano la ugatuzi mjini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu.

Gavana wa Nakuru kwa hasira alitaja matamshi ya Raila kama ya kusikitisha.

Kihika anasema kiongozi huyo wa Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party anastahili kufunga mdomo na kustaafu katika ulingo wa siasa.

Kulingana na Kihika, kiongozi huyo wa ODM alifaa kumsifu Balozi Meg badala ya kukashifu matamshi yake kuhusu uchaguzi wa urais wa 2022.

“Hakupaswa kutumia maneno aliyotumia mchana wa leo, kwa kweli inasikitisha sana kwa mtu wa ngazi yake kumkemea balozi. Labda sasa umefika wakati afunge mdomo na astaafu katika siasa. Ikiwa kweli angesikia kile Whitman aliwasilisha, angeona kwamba yeye sio tu balozi bora wa Kenya lakini balozi mzuri wa Kenya,” Kihika alisema.

Wakati uo huo Kihika amemkosoa  Raila kwa madai ya kuchochea serikali za kaunti dhidi ya utawala wa Rais William Ruto katika usambazaji wa mbolea ya ruzuku unaoendelea kwa wakulima unaoendelea.

Mkuu huyo wa kaunti aliteta kuwa kiongozi huyo wa upinzani alitumia kongamano la ugatuzi kuhujumu baadhi ya mipango ya ushirikiano  baina ya serikali kuu na zile za kaunti.

Kauli ya Gavana Kihika imekuja baada ya Raila Odinga kumkemea Balozi Meg kufuatia tamko lake kwamba rais William Ruto alishinda uchaguzi mkuu 2022 kwa haki.

Wakati wa hotuba yake katika Kongamano la Ugatuzi la 2023, Raila alimkashifu balozi wa Marekani na kumkumbusha kuwa Marekani haikuwa mkoloni wa Kenya.

Kinara huyo wa Upinzani alimwambia balozi Meg afunge mdomo wake na kutishia kushinikiza mswada wa kumtimua Meg katika wadhifa wake humu nchini.

LEAVE A REPLY