Mamlaka ya Kitaifa ya kilimo na chakula nchini Kenya –Agriculture and Food Authority (AFA) inahimiza wakulima kujisajili chini ya mfumo wa kuhifadhi na kudhibiti data za masuala ya kilimo (Kenya integrated Agriculture Management Information System – KIAMS) ili kuboresha zaidi mbinu zao za kilimo.
Katibu mkuu AFA Harsama Kello anasema kuwepo na hifadhi data ya wakulima wote kwenye KIAMS kutarahisisha huduma za kilimo kwa wakulima.
Kello pia anasema hifadhi ya data hiyo itasaidia kutambua uwezo wa kila kaunti na kuanza utaratibu wa usambazaji rasilimali kwa ajili ya kuinukia na miradi ya manufaa zaidi.
“Kuwepo kwa hifadhi data ya kila mkulima katika sehemu moja kutaleta urahisi wa kuweka mipango na mikakati ya uzalishaji wa chakula ndani ya taifa.” Kello alisema katika kongamano lililowaleta pamoja wadau wa maswala ya kilimo kutoka sehemu mbalimbali za taifa, jijini Nairobi.
Mfumo wa KIAMS ulibuniwa chini ya wizara ya kilimo na ustawi wa mifugo kwa madhumuni ya kurahisisha ruzuku kwa wakulima nchini Kenya.
KIAMS pia itasukuma maendeleo ya miradi mbalimbali chini ya wizara ya kilimo na kuhakikisha ongezeko la mavuno, mafunzo ya kilimo ya nyanjani, vyama vya ushirika, masoko na pia uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Serikali ya kitaifa imekuwa mstari wa mbele kuimarisha nguzo muhimu za uboreshaji wa mazao ambazo ni uzalishaji wa vyakula asilia, ufugaji wa wanyama, ng’ombe wa maziwa na ukulima wa maua.
Katika agenda ya kuhakikisha chakula cha kutosha, serikali ya kitaifa imeanzisha mpango wa kutenga ekari elfu 500 za ardhi na kuzifanya kuwa mashamba ya umma kwa ajili ya kukuza chakula.