ELIMU SIO MCHEZO WA PATA POTEA.

0
71

Elimu ni msingi wa maisha ya mwanafunzi na nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote. Masaibu yanayowakumba wanafunzi wa Gredi ya kumi (10) kwa sasa yanaibua hofu kubwa kuhusu mustakabali wa elimu humu nchini.

Licha ya serikali kutangaza kuwa imeongeza maeneo na fursa za kujiunga na Gredi ya kumi (10) , hali halisi ni kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi walioteuliwa hawajajiunga shuleni. Wengine wamekata tamaa kabisa. Sababu kuu ni mzigo mkubwa wa karo na gharama nyingine za kujiunga na gredi ya kumi, ambazo wazazi wengi hawawezi kuzimudu.

Tumeona na kusikia vilio vya wazazi wakilalamika mbele ya kamera na kwenye mitandao ya kijamii, wakiomba kusaidiwa ili watoto wao waweze kuendelea na masomo. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, baadhi ya wanafunzi wameteuliwa kujiunga na shule zilizo nje ya uwezo wa kifedha wa familia zao, hali inayowanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Tahariri hii inasisitiza kwamba elimu nchini Kenya inapaswa kuwa bure kabisa, bila masharti ya kifedha yanayowaumiza wazazi. Fedha za elimu zinapaswa kuwekwa katika mfuko mmoja maalum na kusimamiwa ipasavyo, badala ya kutawanywa kwa wabunge, magavana na viongozi wengine bila uwajibikaji wa wazi.

Iwapo kweli tunataka kuimarisha mfumo wetu wa elimu, lazima tuondoe vikwazo vya kifedha vinavyowanyima watoto wetu fursa ya kujifunza. Elimu bora, ya bure na inayofikika kwa wote si anasa—ni haki. Taifa linalodharau elimu ya watoto wake hujenga msingi dhaifu wa kesho yake.

 

LEAVE A REPLY