Leo nimeamua kuzamia kwenye Bunge letu la Kitaifa taasisi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitajwa kama nguzo kuu ya demokrasia na utawala wa sheria nchini. Lakini swali kuu ni hili: je, bado Bunge letu linafanya kazi kwa niaba ya wananchi au limegeuka uwanja wa maslahi binafsi na michezo ya kisiasa?
Kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa, kumekuwa na miswada kadhaa muhimu ambayo inalenga kuimarisha uwajibikaji na kulinda wale wanaothubutu kusema ukweli mashahidi na wafichuzi wa kashfa za ufisadi. Lakini hadi leo, miswada hii imeendelea kubaki kwenye makabati ya Bunge, ikiangaliwa tu kama kumbukumbu za kale. Ni aibu kubwa kwamba taifa linalojigamba kuwa na katiba imara bado halina sheria madhubuti ya kuwalinda wale wanaopigania haki.
Kinyume chake, tunashuhudia kasi isiyo ya kawaida inapokuwa ni miswada inayohusu maslahi ya wabunge wenyewe iwe ni marupurupu, posho, au maridhiano ya kisiasa. Miswada hiyo hupita kama upepo, bila vizingiti, bila upinzani, na bila kuchelewa. Inashangaza kuona kuwa masuala ya wananchi yanapewa hadhi ya pili, ilhali masuala ya “bosi” na matakwa ya kisiasa hupita kwa urahisi.
Kwa kweli, ni wazi kuwa ndani ya Bunge letu bado kuna wale wabunge wachache wenye moyo wa wananchi. Wanaojitokeza kuunga mkono mageuzi ya kweli. Lakini sauti zao mara nyingi huzimwa na nguvu za kifisadi, hila za kisiasa, na mitandao ya wenye ushawishi mkubwa. Wako wachache, lakini wamedhibitiwa na mfumo ambao unahofia uwazi na ukweli.
Nitasema kwamba ni wakati sasa wa Wakenya kuamka na kudai uwajibikaji. Bunge halipo kwa ajili ya kujilinda, bali kwa ajili ya kulinda wananchi. Miswada inayohusu haki, uadilifu, na uwazi inapaswa kupewa kipaumbele kuliko ile inayowalinda mafisadi.
Bunge letu linapaswa kukumbuka kwamba historia inapoandikwa huandikwa kwa kuwataja. Wale walioweka maslahi ya taifa mbele kuona miswada muhimu kama ile ya kuwalinda mashahidi bado haijapitishwa ni kumsaliti mkenya.
iwapo kuna nia njema ya kupigana na ufisadi basi miswada hiii sharti ipitishwe mara moja nakuwa sheria rasmi ili kuzuia ufisadi Hata ikiwa mashahidi wanaweza kupata ulinzi chini ya sheria ya Witness Protection Act, suala la wabaini wa ufisadi (“whistleblowers”)—yaani watu wanaofichua ukiukaji wa sheria/ufisadi ndani ya shirika au serikalin ilimeonekana kuwa kwa “pengo”. Kwa mfano, taarifa zinaonyesha kwamba hakuna sheria ya kina ya wabaini nchini Kenya.
Kuna mswada wa juu unaojulikana kama Whistleblower Protection Bill (2023/2024) ambao bado haujapita.
Pia kuna “Witness Protection (Amendment) Bill 2023” ambayo inalenga kuboresha sheria ya mashahidi (witness protection) lakini haijakuwa sheria rasmi bado.
Nitamaliza kwa kuuliza wabunge hadi lini tutasubiri sheria hii?



