Bunge la Seneti linatarajiwa kuanza vikao maalum vya siku tatu kusikiza kesi ya kumuondoa afisini Gavana wa Kaunti ya Kericho, Dkt. Erick Kimutai Mutai. Hii ni baada ya wawakilishi wadi wa Kaunti ya Kericho kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye mnamo tarehe 15 Agosti 2025.
Katika kura hiyo ya kutimua gavana huyo, jumla ya wawakilishi wadi 33 kati ya 47 walipiga kura ya ndiyo, hatua iliyofanikisha kuwasilishwa rasmi kwa hoja ya kumbandua Gavana Mutai afisini.
Hoja hiyo iliwasilishwa kwa Bunge la Kaunti tarehe 6 Agosti 2025 na Mwakilishi wa Wadi ya Sigowet-Soin, Rogony Kiprotich. Katika hoja hiyo, Gavana Mutai anashtumiwa kwa matumizi mabaya ya afisi, ukiukaji wa Katiba na taratibu za ununuzi wa umma. Pia anatuhumiwa kwa uteuzi wa kindugu, unyakuzi wa majukumu ya kikatiba na kisheria ya vyombo vya kaunti.
Katika kutetea hoja ya kumbandua Gavana Mutai, Bunge la Kaunti ya Kericho limeunda timu ya mawakili 12 waliobobea katika masuala ya kisheria. Timu hiyo itaongozwa na wakili mashuhuri Elisha Ongoya, ambaye aliwahi kumwakilisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika kesi yake ya kutimuliwa.
Ongoya atasaidiwa na mawakili wengine wakiwemo Kimutai Bosek, Sharon Mibey, Elias Mutuma, Hillary Kiplangat, Brian Langat, Geoffrey Langat na Victor Kibet. Wengine ni Evans Kiplangat, Elvis Kipkorir, Joel Wakhungu, na Vincent Kipronoh.
Aidha, orodha iliyowasilishwa kwa Seneti pia inajumuisha maafisa wanne wa kisheria: Brian Maingi, Ian Kiplangat, Mitchel Mutuma na Japhet Koech.
Wakili Ongoya na Mutuma wanajulikana sana katika mchakato wa mashtaka ya ugatuzi, wakiwa wamehusika katika kesi kadhaa za awali za kutimua viongozi wa kaunti mbele ya Seneti.
Seneti sasa ina jukumu la kusikiza ushahidi wa pande zote na kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya Gavana Mutai kama kiongozi wa Kaunti ya Kericho.



