Nyamira,KENYA
Bunge la Kaunti ya Nyamira limepitisha hoja ya kumwondoa mamlakani gavana wa Nyamira Amos nyaribo baada ya Wajumbe 23 wa Bunge hilo kupiga kura ya ndio kuunga mkono hoja hiyo .
Hoja hiyo, ililetwa na mwakilishi Wadi ya Bonyamatuta, Julius Matwere ambayo imeelezwa kama jaribio pana zaidi na lenye uzito mkubwa kuliko yote yaliyowahi kufanywa dhidi ya Gavana Nyaribo. Kupitia hoja hiyo, wawakilishi wadi wametaja orodha ndefu ya tuhuma dhidi ya gavana, wakimshutumu kwa ukiukaji mkubwa wa Katiba ya 2010, matumizi mabaya ya mamlaka, na kukiuka kanuni muhimu za ugatuzi.
Gavana Nyaribo amepitia majaribio mawili ya awali ya kuondolewa kiujumla lakini akaepuka zote hizo kwa kura chache. Hata hivyo, safari hii ameangushwa na Bunge la Kaunti na sasa hatima yake iko mikononi mwa Seneti, ambayo itapokea mashtaka hayo na kufanya uchunguzi wake kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.
Hoja za kubanduliwa mamlakani ni madai yanayohusu fedha za umma na usimamizi katika serikali ya kaunti. Tuhuma kuu ni ile ya KSh 32 milioni zinazodaiwa kupotea kupitia udanganyifu wa malipo ya watumishi (payroll fraud). MCAs wanasema kwamba mpango huo uliundwa ili kuelekeza fedha za kaunti kwa washirika wa gavana kupitia uingizaji wa majina hewa kwenye orodha ya malipo.
Inadaiwa pia kuwa Gavana Nyaribo alinufaika binafsi kupitia malipo yasiyo ya kawaida ya KSh 5,649,706 kama madai ya arrears ya mshahara, kinyume cha taratibu za kifedha.
Hoja hiyo inashutumu zaidi hatua za gavana kufanya uteuzi bila ridhaa ya Bunge la Kaunti, ikiwemo kumteua CEC na wanachama wa kamati ya uteuzi ya CPSB bila kufuatwa kwa taratibu za kisheria.
wawakilishihao hao wanadai kuwa gavana alijaribu kunyakua mamlaka ya Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti (CPSB) kupitia ukaguzi haramu wa payroll, kuwapunguza vyeo baadhi ya watumishi, na hata kudaiwa kujaribu kumsimamisha kazi Katibu wa Bodi hiyo bila uwezo wa kisheria.
Kwa kupitishwa kwa hoja hiyo, mchakato sasa utahamia Seneti ambapo mashtaka yote dhidi ya Gavana Nyaribo yatawasilishwa rasmi kwa uchunguzi wa kina. Seneti ndiyo sasa ina uwezo wa kumwondoa kabisa au kumrejesha mamlakani baada ya kupitia ushahidi na kuskiliza pande zote.



