Bunduki za Serikali Dhidi ya Raia Wake

1
86

‎Mwaka haujaenda mbali. Bado tuko Januari, lakini tayari taifa limeshuhudia visa zaidi ya vitatu vya raia kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi. Polisi ambao, kwa mujibu wa katiba na kiapo cha kazi yao, wanapaswa kuwalinda raia na mali zao. Badala yake, baadhi yao wamegeuka kuwa chanzo cha hofu, majonzi na simanzi kwa wananchi.

‎Na si mauaji pekee. Majuzi tu, taifa lilishuhudia tukio la kugathabisha katika Kaunti ya Nandi ambapo polisi waliwashambulia na kuwatandika raia waliokuwa wanacheza mchezo wa (pool table)
‎Hawa hawakuwa wahalifu, hawakuwa wamejihami, bali walikuwa raia wakijihusisha na burudani yao.
‎Swali kuu basi linabaki palepale;

‎Je, ni swala la afya ya akili miongoni mwa baadhi ya maafisa wa polisi? Au ni matokeo ya mafunzo duni hasa katika udhibiti wa hasira, mawasiliano na matumizi ya nguvu kwa uwiano unaokubalika? Ama tumefika mahali ambapo baadhi ya askari wamezoea kutumia nguvu kama suluhu ya kwanza, wakijua kuwa mara nyingi hakuna uwajibikaji wa kweli unaofuata?

‎Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zinaonyesha mwelekeo unaotia wasiwasi raia wanapigwa risasi, wanapigwa virungu, wanadharauliwa hadharani na yote haya yakifanywa na watu wale wale waliokabidhiwa jukumu la kuwalinda. Familia zinabaki na vilio, jamii zinaishi kwa hofu, na imani ya umma kwa vyombo vya usalama inaendelea kuyeyuka.

‎Tahariri inasema kwamba ni wakati wa wizara ya Usalama wa Ndani kujitokeza wazi na kutoa majibu kwa wananchi:
‎Je, wizara ina mkakati gani wa kushughulikia afya ya akili ya maafisa wa polisi?Je, mafunzo yanayotolewa yanawajenga askari wanaojua kudhibiti hasira na kuheshimu haki za binadamu?Kwa nini matumizi ya nguvu kupita kiasi yanaendelea kana kwamba ni jambo la kawaida?

‎Vilevile Idara ya Polisi (NPS)lazima ijitathmini kwa dhati. Je, mifumo ya nidhamu ipo kwa vitendo au ni kwenye makaratasi tu? Askari wanaokiuka sheria wanachukuliwa hatua zipi, au sare na bunduki vimekuwa kinga dhidi ya haki?

‎Hatimaye IPOA Idara Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi. IPOA lazima isimame imara, ichunguze kwa haraka, kwa uwazi na bila upendeleo matukio haya yote kuanzia mauaji ya raia hadi ya polisi wengine.

1 COMMENT

  1. Mie mtazamo wangu naona ni afya ya akili au ma askari wanajiona wao wapo juu ya sheria e.g unaeza kaa nje kwako usiku unapunga unyunyu mara ma askari kwenye patrolling zao wanakukuta na kukuharass uingie ndani kana kwamba wao ndio wanamiliki dunia aah hii tabia inachosha sana na ukijaribu kuwaelezea utaambulia kipigo sana & huu ni wakati idara zote husika wakae chini na kutathmini mambo kama haya manake Raia tunaishi kwa hofu hasa tukiona askari mwenye ameenda mafunzo lakini Cha kushangaza mafunzo yamepotea kwenye sikio la kulia kuenda kushoto na istoshe afadhali ukutane na jambazi njiani anaeza kukusamehea kuliko ukutane na afisa wa usalama huponi na ukiponea ujue hapo ushaacha kakitu almaarufu ( HONGO )

LEAVE A REPLY