Ugatuzi Na Hali Halisi Kaskazini Mwa Kenya

0
90

Ugatuzi, kama ulivyowekwa katika Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, haukuwa mapambo ya kisheria wala ahadi ya kisiasa. Ulilenga jambo moja kuu kupeleka maendeleo karibu na wananchi. Ulilenga kurekebisha dhuluma za kihistoria, kuhakikisha kila eneo la nchi linapata rasilimali, huduma na fursa sawa za maendeleo.

Ndiyo maana kauli ya aliyekuwa Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua kwamba viongozi wa kaskazini ya Kenya warudi nyumbani wafanye maendeleo, imeibua mjadala mzito lakini wa lazima. Kauli hii, iwe mtu anaipenda au haipendi, inalazimisha taifa kujiuliza maswali magumu kuhusu uwajibikaji wa ugatuzi.

Tahariri inauliza Ugatuzi ni nini hasa? Ugatuzi maana yake ni pesa, mamlaka na maamuzi kushuka chini hadi ngazi ya kaunti. Shule bora kwa watoto wetu, Barabara za kuunganisha jamii na masoko, Hospitali zinazofanya kazi,Vituo vya polisi vinavyolinda raia Kwa kifupi, ugatuzi ni maendeleo yanayoonekana kwa macho, si ripoti nzuri kwenye makaratasi ya ofisini.

Maeneo ya kaskazini mwa Kenya kwa miaka mingi yalikuwa yakitajwa kama yaliyotengwa na maendeleo. Lakini tangu kuanza kwa ugatuzi, mabilioni ya pesa hutumwa kila mwaka kwa kaunti hizi kupitia mgao wa ugatuzi, NG-CDF na fedha za usawazishaji.

Lakini swali linaloendelea kuulizwa na wananchi ni kwamba Pesa hizi zinaenda wapi? Kwa nini bado kuna Shule ambapo watoto wanasoma chini ya miti au kwenye madarasa ya matope? inasikitisha kugundua kwamba kuna maeneo ambayo hayajawahi kuona hata kilomita moja ya barabara ya lami, zipo hospitali zisizo na vifaa, dawa au wahudumu wa kutosha?

Wakati huo huo, kuna maeneo mengine ya nchi yanayoendelea kushuhudia barabara za lami, shule za kisasa na miundombinu bora mwaka baada ya mwaka.

Kauli ya Rigathi Gachagua haikuwa tu ya kisiasa ilikuwa changamoto kwa viongozi wa kaunti za kaskazini akiwataka wawajibike na kuhakikisha pesa wanazopokea zinaleta mabadiliko kwa wananchi wao.

 

LEAVE A REPLY