CDF na Elimu: Wakati wa Kufunga Mlango wa Siasa Mashuleni

0
224

Kwa miaka mingi, elimu imekuwa silaha ya kisiasa. Wanasiasa wanapofika mashinani kuomba kura, huahidi bursaries, madarasa na misaada mbalimbali, kana kwamba elimu ni hisani ya kisiasa badala ya haki ya msingi. Ndiyo maana tunajiuliza: mbona fedha zote za elimu zisikusanywe kwenye hazina moja?

 

Leo, Wizara ya Elimu hutengewa mamia ya mabilioni ya shilingi kila mwaka. Pamoja na hayo, kuna mabilioni mengine yanayopita kwa mikono ya wabunge kupitia CDF, yakitumika kugawa bursaries na miradi midogo ya elimu. Fedha hizi zikiunganishwa katika mfuko mmoja wa kitaifa, elimu ya bure bila malipo ingekuwa jambo linalowezekana kabisa.

 

Tukitazama nchi kama Singapore, mafanikio yake hayakujengwa kwa siasa za bursaries bali kwa mfumo mmoja thabiti wa elimu, unaosimamiwa kitaifa, unaofadhiliwa ipasavyo, na unaolenga ubora, nidhamu na usawa. Ndiyo maana Singapore leo ni kitovu cha maarifa, teknolojia na uchumi imara.

 

Moja ya changamoto kubwa ni kwamba fedha hizi za NG-CDF mara nyingi huonekana kutumika zaidi kwa maslahi ya kisiasa kuliko maendeleo ya elimu kwa msingi imara. Wabunge hujitahidi kuonyesha mafanikio ya kugawa bursaries au kujenga madarasa wakati wa kampeni, badala ya kuweka mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha elimu bora na bure kwa wote

 

Ikiwa kweli tunataka kufikia kiwango cha Singapore, lazima tuache kutumia elimu kama chambo cha kura. Elimu iwe sera ya taifa, si mradi wa mbunge. Hazina moja, usimamizi mmoja, na dhamira moja elimu bora na bure kwa kila mtoto.

 

LEAVE A REPLY