Kiburi Cha Mamlaka Ni Dalili za Udikteta Mpya

0
92

Huenda wengine wakasema Kenya haina tatizo la ukoloni mamboleo, lakini ishara za hatari hii zimeanza kujitokeza waziwazi. Wakati taifa letu likijigamba kwa demokrasia, ukweli ni kwamba vitendo vya baadhi ya viongozi vinaonyesha dalili za udikteta unaokua taratibu.
Tumewasikia washirika wakuu wa serikali wakitamka hadharani kwamba, wakenya wapende wasipende, Rais William Ruto atatawala hata baada ya mwaka 2027. Kauli kama hizi sio za mzaha. Ni matamshi yanayodhihirisha kiburi cha mamlaka na dharau kwa wananchi ambao wanaotakiwa kuwa chanzo cha nguvu za serikali kwa mujibu wa Katiba.

Tumewaiwasikia washirika wa serikali na wengine kwa uwazi kwamba Rais Dkt. William Ruto, anapaswa kuondolewa ukomo wa mihula ya urais ili atawale zaidi Wengi wetu tunaweza kupuuzilia mbali madai hayo tukiyachukulia kama uvumi, lakini historia imetufundisha kwamba mambo makubwa huanza kwa uvumi. Mara nyingi, uvumi huo huwa ni njia ya dola kupima joto la wananchi kujaribu kuona kama hasira za umma zitapasuka au tutanyamaza kimya.

Vilevile, tumemsikia Kiongozi wa Wengi Bungeni akijivunia kwamba Bunge lilipitisha miswada ya kifedha iliyokataliwa vikali na kizazi cha Gen Z mwaka 2024, na iliyosababisha maafa makubwa. Alifichua kuwa waligawa mswada huo katika vipande vinne vidogo na kuupitisha kimyakimya. Kauli kama hizi si za kufurahisha, bali ni kielelezo cha kiburi na dharau kwa demokrasia. Serikali inapoanza kujiona iko juu ya wananchi, hapo ndipo ukoloni mamboleo unapoanza kuota mizizi.

Tumeona pia juhudi za kupitisha sheria ya kudhibiti mitandao ya kijamii, ikipigiwa upatu na wafuasi wa serikali. Ni wazi kwamba mitandao imekuwa kama upinzani mpya jukwaa ambalo wananchi, hasa vijana, hutumia kusema ukweli bila woga. Badala ya kuzingatia sauti hizi kama njia ya kujirekebisha, serikali imechagua kuziona kama tishio linalopaswa kudhibitiwa.

Hali hii inatukumbusha enzi za ukoloni, ambapo mkoloni aliamua kila kitu kwa niaba ya raia na akapiga marufuku yeyote aliyethubutu kuhoji mamlaka. Tofauti pekee sasa ni kwamba mkoloni amevaa ngozi nyeusi na anatoka miongoni mwetu. Huyu ndiye mkoloni wa kisasa anayetumia wadhifa wake na vyombo vya dola kutunyamazisha na kututisha.
Leo hii nitasema kwamba pamoja na uhuru wa kujieleza ulioandikwa kwenye Katiba, inazidi kuonyesha tabia za mataifa ya kidhalimu. Matumizi ya nguvu, utekaji, mashtaka ya kubuni na uundaji wa sheria kandamizi kwa siri, yote yanaonyesha kwamba uhuru wetu uko mashakani

Ni lazima tuamke. Uhuru si tukio lililotokea mwaka 1963 – ni mchakato unaohitaji kulindwa kila siku. Wananchi lazima wakumbushwe kwamba mamlaka ni yao, na viongozi wawakilishi wa muda tu. Tukinyamaza sasa, tutakuwa tumekubali kurudi kwenye minyororo – safari hii, mikononi mwa ndugu zetu wenye ngozi sawa nasi.

LEAVE A REPLY