KAMATI YA MOMBASA YA VOICE FOR PALESTINE KUANDAA MATEMBEZI NA UPANDAJI MITI KWA AJILI YA GAZA

0
68

 

Kamati ya Voice for Palestine (VFP) ya Mombasa imetangaza mpango wa kufanya matembezi ya mshikamano na shughuli ya upandaji miti kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wa Gaza wanaokabiliwa na janga la kibinadamu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamati hiyo, matembezi hayo yatafanyika siku ya Jumamosi, tarehe 8 Novemba 2025, yakianzia Mapembeni, kupitia Treasury Square na kuhitimishwa katika Mchanga wa Mama Ngina Waterfront, ambako shughuli ya upandaji miti itafanyika.

Tukio hilo linaandaliwa kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Mombasa na linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mashuhuri wa dini ya Kiislamu, wanasiasa na viongozi wa maoni kutoka Pwani na maeneo mengine nchini.

Wakati wa kikao cha mashauriano kilichofanyika katika Ukumbi wa Afraha, karibu na Kituo cha Polisi cha Mbaraki, Sheikh Ahmed aliwataka Wakenya wa madhehebu na makabila yote kushiriki kwa wingi katika tukio hilo.

“Leo tumeungana hapa Mombasa na kauli moja kwa taifa zima kuwa tarehe 8 Novemba tutakusanyika kwenye Mchanga wa Mamangina. Tunawaalika wote, bila kujali uko nani, kujiunga nasi kwa mshikamano na ndugu zetu huko Gaza,” alisema Sheikh Ahmed.

Aliongeza kuwa mkusanyiko huo utakuwa ishara ya mshikamano na watu wa Gaza, sambamba na uzinduzi wa Mpango wa Upandaji Miti kwa Mkoa wa Pwani, ambapo zaidi ya miti 10,000 itapandwa.

“Tutakuwa tukikusanya fedha kwa ajili ya misaada ya matibabu, na wakati unaofaa tutarudi na kupanda miti hiyo hapa Mombasa,” aliongeza Sheikh Ahmed.

Kamati ya waandaaji imesisitiza kuwa tukio hilo ni la wazi kwa kila mtu, bila kujali dini au asili, na imewahimiza wananchi wote kushiriki katika harakati hizo za kibinadamu na mazingira.

 

LEAVE A REPLY