Kwanini Migongano Kati ya Huduma Kuu za Usalama?

0
67
PICHA /maafisa wa polisi

‎Kuahirishwa kwa ghafla kwa zoezi la uajiri wa maafisa wa polisi ni pigo kubwa kwa maelfu ya vijana waliokuwa wamesubiri kwa hamu fursa hii ya ajira. Lakini zaidi ya hayo, linaloibua wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya utawala ndani ya vyombo vyetu vya usalama.

‎Ni aibu kwa taifa kuona taasisi mbili zinazopaswa kushirikiana kwa karibu yaani, afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi na Tume ya Huduma ya Polisi zikiwa katika mvutano unaohusiana na masuala nyeti kama mishahara ya maafisa. Hali hii inatuma ujumbe mbaya kwa raia na kwa wale wanaotarajia kujiunga na huduma ya polisi.

‎Ikiwa viongozi wa usalama hawawezi kukubaliana kuhusu maslahi ya maafisa waliopo na wanaotarajiwa, ni vipi basi watatoa huduma bora kwa wananchi? Ni muhimu kwa viongozi husika kuacha tofauti zao na kutanguliza maslahi ya taifa. Aidha, uaminifu wa umma kwa vyombo vya usalama hauwezi kudumishwa iwapo kuna migongano ya mara kwa mara ndani ya taasisi hizi.

‎Serikali inapaswa kuingilia kati haraka iwezekanavyo ili kusuluhisha mvutano huu na kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata haki yao ya kuajiriwa kwa njia ya haki, wazi, na isiyo na doa.

‎Wakati umefika kwa taasisi hizi kufanya kazi kwa mshikamano, kwa sababu usalama wa taifa hauwezi kuwa mateka wa migongano ya kiuongozi.Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) ina mamlaka ya kushughulikia masuala ya kiutumishi kama ajira, kupandisha vyeo, nidhamu, na mishahara ya maafisa wa polisi.

‎Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) ana mamlaka ya kuongoza operesheni za kila siku za polisi, kuhakikisha usalama, na kusimamia utendaji wa maafisa wake.
‎Kwa hivyo, kwa misingi ya kikatiba, hakutakiwi kuwa na mzozo kuhusu nani anasimamia mishahara hiyo ni kazi ya NPSC kwa mujibu wa sheria. IG hana mamlaka ya kupanga mishahara, isipokuwa kutoa maoni ya kiutendaji.

‎Lakini, kwa nini basi kuna mzozo?
‎Hapa ndipo maswali ya kina yanaibuka:
‎Je, kuna mapambano ya madaraka kati ya NPSC na IG?
‎Inawezekana kuwa Inspekta Jenerali anahisi kuwa Tume inavuka mipaka na kuingilia masuala ya kiutendaji, au pengine anataka ushawishi zaidi katika masuala ya kiutumishi ili aweze kuwa na udhibiti kamili wa maafisa wake.

‎Je, kuna masuala ya matumizi ya fedha yanayofichwa?
‎Ikiwa mishahara ni kisingizio, basi huenda kuna ukakasi kuhusu bajeti, posho, au mwelekeo wa fedha za umma zinazotengwa kwa polisi. Viongozi wanaweza kupigania udhibiti wa fedha hizo kwa sababu mbalimbali zisizotajwa hadharani.
‎Je, kuna mvutano wa kisiasa au maslahi binafsi?

‎Katika baadhi ya visa, viongozi wa taasisi huteuliwa kwa msingi wa kisiasa. Migongano ya kiutendaji inaweza kuwa kielelezo cha mvutano mkubwa zaidi wa kisiasa au kimamlaka ndani ya serikali.

‎Je, kuna ukosefu wa mawasiliano au tafsiri tofauti za sheria?
‎Wakati mwingine taasisi mbili zinaweza kuwa na tafsiri tofauti za majukumu yao kikatiba. Bila maelewano ya wazi, tofauti hizi huzaa mvutano mkubwa.

‎Kwa hali ilivyo sasa, mvutano huu unazua maswali mengi kuliko majibu. Iwapo ni mishahara tu, basi suluhisho lingepatikana haraka kwa kufuata Katiba na sheria. Lakini kwa kuwa suala hili limezua malumbano ya wazi na kufikisha jambo mahakamani, ni wazi kuwa kuna kina zaidi cha kisiasa, kiutawala au kifedha kinachochochea mgogoro huu.

LEAVE A REPLY